📍 Chake Chake, Kusini Pemba
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kumaliza tatizo la usafiri na usafirishaji wa mizigo katika Kisiwa cha Pemba.
Ameyasema hayo leo alipoufungua Msikiti mpya wa Chachani, uliojengwa na mfanyabiashara Ndg. Said Nassor Bopar.
Rais Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa tayari Serikali imeandaa meli mbili za mwendo kasi kukabiliana na uhaba wa vyombo vya usafiri kwa wananchi wa Pemba, sambamba na mipango ya kutafuta meli maalum ya mizigo itakayofanya safari kati ya Unguja na Pemba.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeliagiza Shirika la Meli la Zanzibar kushiriki kikamilifu katika huduma za usafiri baharini badala ya kuiachia sekta binafsi pekee, huku akibainisha kuwa meli ya MV Mapinduzi (2) itaanza kufanya kazi hivi karibuni baada ya kukamilika kwa matengenezo yake.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa bandari za Pemba kutachochea uwekezaji wa sekta binafsi na kuongeza vyombo vya usafiri, hatua itakayosaidia juhudi za Serikali za kumaliza changamoto hiyo kwa wananchi.
Katika nasaha zake, Alhaj. Dkt. Mwinyi amewaasa waumini kuitumia misikiti kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto za makundi maalumu wakiwemo wajane, mayatima na wasio na uwezo.
Amempongeza Ndg. Said Nassor Bopar kwa kujenga msikiti huo na kuwahimiza wenye uwezo kuwekeza katika mambo ya kheri.
Vilevile, amewasisitiza wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa wakati wa Ramadhan na kuwataka waumini kuzidisha ibada na kuhurumiana.



