Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kuiboresha Bandari ya Tanga ili iweze kukidhi ushindani wa kibiashara uliopo katika bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi.
Akizungumza Februari 16, 2026 wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa bandari ya Tanga, Dkt. Nchemba amesema maboresho yanayoendelea ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuimarisha sekta ya bandari nchini.
Amesema awamu ya pili ya maboresho ya Bandari ya Tanga, itahusisha ujenzi wa gati mbili mpya ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena na meli kubwa zaidi.
Amesema maboresho hayo yanalenga kuboresha huduma za kibandari na kukidhi mahitaji ya soko, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, amesema mikakati ya kuendeleza maboresho ya Bandari ya Tanga inaakisi dhamira ya dhati ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha sekta ya uchukuzi na kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mha. Dkt. Baraka Mdima, akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Bw. Plasduce Mbossa, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maboresho ya bandari mbalimbali nchini, zikiwemo bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi pamoja na bandari za maziwa, akisisitiza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi na ushindani katika sekta ya usafirishaji wa mizigo.












