Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,
Dar es Salaam

POLISI wametia mguu katika Ofisi za Makao Makuu ya Chama Cha Wananchi (CUF) zilizopo Buguruni na kuweka ulinzi mkali kufuatia kundi la watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa chama hicho kuingia wakiwa na mabango na matarumbeta.

Kundi hilo liliingia ofisini hapo kwa hali isiyotarajiwa likiwa na mabango ya kumpongeza Msajili wa Vyama vya Siasa kwa uamuzi wake wa kutengua uongozi uliopo madarakani chini ya Profesa Ibrahimu Lipumba, wakidai ulikiuka kanuni za uchaguzi za katiba yao ya chama.

Dakika chache baada ya kundi hilo kuingia, gari la Polisi aina ya Land Cruiser Pick-up lenye namba za usajili PT 4854, likiwa na askari kadhaa wenye silaha, liliwasili eneo hilo na kutanda ndani ya ofisi hizo.

Askari kiongozi alizungumza na wanachama hao kabla ya kuelekea ukumbini ambako Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya, alikuwa akizungumza na waandishi wa habari alimwambia;

“Sakaya, nataka utulivu hapa nimekuwa na wewe kwenye kampeni bila kuona vurugu, nitashangaa hapa nikiona vurugu nimepigiwa simu kwamba hapa kuna moto unawaka, ndiyo maana tuko hapa. Tunataka utulivu.” alisema Polisi.

Kabla ya tukio hilo, Sakaya alipinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kutengua uongozi uliopo unaoongozwa na Ibrahim Lipumba.

Katika mkutano huo, Sakaya alisema chama hicho kinakusudia kwenda mahakamani kutafuta haki ya kikatiba kufuatia uamuzi huo.

“Hiki si chama cha kwenye majani, ni chama cha ukombozi na kina katiba. Hivyo Msajili hawezi kutuingilia. Tunakwenda mahakamani kutafuta haki,” alisema Sakaya.

Aliongeza kuwa wanachama wa CUF hawawezi kuchaguliwa viongozi na Msajili wa Vyama vya Siasa, akidai hatua hiyo inaweza kusababisha mgogoro ndani ya chama.

“Kwa kufanya hivyo watakuwa wanaleta vurugu. Tunaamini wanataka kukiua chama hiki kama walivyokiua NCCR Mageuzi na vingine vikubwa hapa nchini,” alisisitiza.

Chanzo cha Mgogoro
Msuguano huo unatokana na barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyopokelewa na CUF Februari 13 mwaka huu, ikikitaka chama hicho kurejea uchaguzi mkuu wa ndani uliofanyika Desemba 2024.

Uchaguzi huo ulimrejesha madarakani Profesa Lipumba, lakini ulidaiwa kukiuka kanuni kutokana na kutofikiwa kwa asilimia 50 ya wapiga kura wote.

Sakaya alihoji ni kwa nini ofisi ya Msajili haikuchukua hatua kwa kipindi chote cha miaka miwili iliyopita, hadi sasa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama waliodaiwa kufukuzwa.

Alisema katika uchaguzi huo Msajili alikuwepo na aliubariki, jambo linalowafanya kushangazwa na hatua hiyo ya sasa.