Na John Walter, JamhuriMedia, Babati

Mkuu wa Wilaya ya Babati na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, Emmanuela Kaganda, amesema wanafunzi waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kumshambulia mwenzao hadi kufariki dunia wameachiwa huru na sasa wanaendelea na maisha yao ya kawaida.

Akizungumza wakati akihitimisha hotuba yake katika hafla ya kuwapongeza walimu waliofundisha kidato cha nne mwaka 2025 katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati kwa kufanikisha matokeo mazuri ya wanafunzi, Kaganda ameupongeza uongozi wa Jeshi la Magereza Wilaya ya Babati kwa mchango wao katika malezi na elimu ya wanafunzi hao.

Amesema kulikuwa na wanafunzi waliokinzana na sheria na kuhifadhiwa katika mazingira ya uangalizi maalum, akitolea mfano tukio lililotokea katika Shule ya Sekondari Qash, ambapo wanafunzi hao waliendelea kupata fursa ya kusoma na kufanya mitihani yao chini ya usimamizi wa karibu wa maafisa elimu, uongozi wa magereza na walimu.

“Kuna watu waliona lile ni eneo baya, lakini ni eneo la urekebishaji, watoto wamekaa pale, wamesoma na kufanya vizuri katika mitihani—wapo waliopata daraja la kwanza na la pili, hakuna aliyepata sifuri, kama wangetelekezwa tungewanyima haki yao ya msingi ya elimu,” alisema Kaganda.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya ofisi ya elimu, Jeshi la Magereza na walimu uliwezesha wanafunzi hao kufanya mitihani kwa mafanikio, na sasa wameachiwa huru na wanaendelea na masomo na maisha yao kwa utulivu.


Mnamo Agosti 16, 2025, zaidi ya wanafunzi kumi walikuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kumuua mwenzao, Yohana Konki (17), kwa madai ya wizi wa kishkwambi, tukio lililoshtua jamii ya Wilaya ya Babati.