Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umekabidhi jengo la kisasa la karakana ya uchomeleaji pamoja na vifaa vya mafunzo kwa Chuo cha Ufundi Stadi cha Don Bosco jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Msaada huo unalenga kuimarisha mazingira ya kujifunzia kwa vitendo na kuongeza ubora wa mafunzo ya ufundi stadi, hususan katika fani ya uchomeleaji ambayo ina mahitaji makubwa katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkurugenzi wa Mradi wa EACOP, Bw. Emmanuel Blarez, alisema kuwa miongoni mwa vipaumbele vya mradi huo ni kusaidia jamii kwa kuwekeza katika sekta ya elimu na maendeleo ya ujuzi.

“Tunaunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika miradi mbalimbali ya Serikali na sekta binafsi, ndani na nje ya nchi. Hivyo, uwekezaji huu katika elimu ya ufundi ni uwekezaji muhimu kwa maendeleo ya taifa,” alisema Bw. Blarez.

Aliongeza kuwa jengo hilo pamoja na vifaa vilivyokabidhiwa ambavyo vitawawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira salama, bora na yanayokidhi viwango vya kisasa, hali itakayowavutia wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kozi ya uchomeleaji.

“Nawasihi wanafunzi kulitumia vyema jengo hili na vifaa mlivyopata ili mjijengee umahiri utakaowafanya kuwa washindani katika soko la ajira. Nidhamu, ujuzi na kujituma ni nguzo muhimu za mafanikio,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Don Bosco, Padre Felix Wagi, aliushukuru mradi wa EACOP kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo sera ya fursa kwa wazawa kupitia uwekezaji katika elimu na kuwawezesha vijana kiuchumi na kitaaluma.

Alisema maboresho hayo yataongeza idadi ya wanafunzi katika kozi ya uchomeleaji, ambayo awali ilikuwa na wanafunzi kati ya 15 hadi 20 pekee kutokana na changamoto za miundombinu.

“Kwa maboresho haya, tunaamini idadi ya wanafunzi itaongezeka kwa kiasi kikubwa na tutazalisha wataalamu wengi zaidi watakaohitajika katika miradi mikubwa ya kitaifa na kimataifa,” alisema Padre Wagi.

Meneja wa Uwajibikaji na Uwezeshaji wa EACOP Tanzania, Bi. Clare Haule, alisema mradi unatambua umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya vijana kama chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa. Alibainisha kuwa uamuzi wa kusaidia idara ya uchomeleaji ulitokana na tathmini iliyofanyika miaka miwili iliyopita ambayo ilionesha hitaji la kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Tulivutiwa na hamasa na utayari wa wanafunzi licha ya changamoto za miundombinu. Hilo ndilo lililotupa moyo wa kushirikiana na uongozi wa chuo hiki kuboresha mazingira haya,” alisema Bi. Haule.

Aliwataka wanafunzi kuthamini na kutumia ipasavyo vifaa hivyo, akieleza kuwa fursa kama hiyo ni nadra na inaweza kuwa daraja la kufikia ndoto zao za kitaaluma na kimaisha.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki, Bw. Lorivii Longidu, aliipongeza EACOP kwa kuendelea kuwa kinara katika utekelezaji wa sera ya Taifa ya fursa kwa wazawa kwa kugusa maisha ya jamii na kuwainua vijana kupitia mafunzo ya ujuzi.

“Uwekezaji huu hauwanufaishi wanafunzi wa Don Bosco pekee, bali Taifa zima. Wahitimu hawa watakapomaliza masomo yao, watachangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo ama kwa kuajiriwa au kujiajiri,” alisema.

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Bw. Casmir Joseph, alisema jengo na vifaa vilivyotolewa vitaongeza ari ya kujifunza kwa vitendo na kuhamasisha vijana wengi zaidi, wa kike na wa kiume, kujiunga na masomo ya ufundi stadi.

Mradi wa EACOP wenye urefu wa kilometa 1,443 unatoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, mkoani Tanga, ukipitia mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.

Wanahisa wa mradi huo ni TotalEnergies (asilimia 62), TPDC (asilimia 15), Uganda National Oil Company – UNOC (asilimia 15) na China National Offshore Oil Corporation – CNOOC (asilimia 8).