Na Mwavua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, imekanusha taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa JamiiForums ikidai kuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ruvu Station wanasomea katika madarasa yaliyoezuliwa paa.
Regina Bieda alifafanua kuwa ni kweli baadhi ya madarasa yaliezuliwa paa kufuatia athari za kimbunga kilichotokea hivi karibuni.
Hata hivyo, alieleza kuwa mara baada ya tukio hilo, hatua za haraka zilichukuliwa na wanafunzi kuhamishiwa katika madarasa mengine ndani ya shule hiyo.
Majengo yote yaliyoathirika hayatumiki kwa shughuli za ufundishaji tangu yalipoathirika, ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi na walimu.
Aidha, Halmashauri hiyo imesisitiza kuwa Shule ya Sekondari ya Ruvu Station haina upungufu wa vyumba vya madarasa, na mchakato wa utoaji elimu unaendelea kama kawaida bila kuathiriwa na tukio hilo.
Halmashauri imewataka wananchi kupuuza taarifa zisizo sahihi na kuzingatia taarifa rasmi zinazotolewa na mamlaka husika.





