Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Manyoni
Kesi ya Jinai Na. 3454/2026 imefunguliwa Februari 18, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida, dhidi ya Bw. Herbert Matiko Tugara, Mzabuni wa Kampuni ya ‘Herver General Services’.
Mshtakiwa anakabiliwa na shtaka la kutoa nyaraka za uongo kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (Marejeo ya mwaka 2022), pamoja na shtaka la kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya mwaka 2022).
Mshtakiwa anadaiwa kughushi risiti ya EFD yenye thamani ya shilingi 6,200,000/= na kuiwasilisha kama nyaraka halali baada ya kupokea malipo ya kazi ya usambazaji wa vifaa vya umeme katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni iliyokuwa inakarabatiwa.
Mashtaka hayo yalisomwa mahakamani na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Wilson Ntiro, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, Mhe. Itika Koroso.
Mshtakiwa alikana mashtaka yanayomkabili na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama.
Kesi hiyo imepangwa tarehe 2 Machi 2026 kwa ajili ya kusoma hoja za awali na kuanza usikilizwaji.


