Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Babati
WANAWAKE wadau wa madini wa Mkoa wa Manyara, wamesherehekea Siku ya Wanawake duniani kwa kuwatembelea na kuwapa vyakula na nguo wazee wasiojiweza wanaolelewa katika kituo cha Magugu Wilaya ya Babati.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini Tanzania (TAWOMA) Rachel Njau amesema wanawake hao wadau wa madini wamewapatia zawadi tofauti za thamani ya shilingi milioni 1.875.
Rachel amesema wamewanunulia wazee hao zawadi mbalimbali ikiwemo mablanketi, mashuka mazito ya kulalia, nguo, mafuta ya kupikia, mchele, unga na sabuni.
Amesema wametekeleza hayo baada ya Mkuu wa Mkoa huo Queen Sendiga alipofanya ziara kwenye machimbo ya madini ya Tanzanite hivi karibuni na kuwaasa wachimbaji wawatembelee wazee hao.
“Mkuu wetu wa mkoa alipotembelea Mirerani hivi karibuni alieleza juu ya wachimbaji kuwatembelea wazee hawa wa Magugu na leo tumetekeleza hilo kwa kuwaona na kuwapa baadhi ya mahitaji,” amesema Rachel.
Mwenyekiti wa wafanyabishara wanawake wa Magonga ya Tanzanite Mirerani, Magreth Nelson amesema wameungana wanawake wadau wa madini ili kuwapa upendo wazee hao.
“Hakuna tulicholeta zaidi ya upendo kwa wazee wetu, sisi baada ya kusikiliza nasaha za Mkuu wetu wa Mkoa kwamba kuna wazee wanalelewa na Serikali hapa Magugu ndipo tukafika kuwaona,” amesema Magreth.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali, taasisi, mashirika na watu binafsi kuwatembelea wazee hao na kuwapa misaada.
Ofisa mfawidhi wa makazi ya wazee na wasio jiweza Magugu, Maige Jackson amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 1974.
Jackson amesema kituo hicho kinaendeshwa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kina wazee tisa, wakiwemo wanaume saba na wanawake wawili.
Mwenyekiti wa wazee wa kituo hicho Mathias Jacob amewashukuru wanawake hao kwa kuwatembelea na kuwapa zawadi mbalimbali ikiwemo nguo na vyakula.
“Tunawashukuru wakina mama hawa kwa kututembelea na kutupa zawadi, tunasema asante sana Mungu awabariki,” amesema Jacob.
Mzee mwingine wa kituo hicho, Danasian John amewashukuru wanawake hao kwa kufika kwenye kituo chao Magugu na kuwasalimia na kuwapa zawadi ya vyakula na nguo.
“Mama zangu mmesema kuwa hiki mlichotupa ni kidogo hapana kwetu ni kikubwa mno na tunawashukuru kwa kuja,” amesema John.


