Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mkuranga

Jumla ya sh bilioni 6.8 zimetumika katika ufadhili wa mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani katika mikoa ya Lindi na Pwani.

Hayo yamebaiika leo Machi 8, 2026 wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyowashirikisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya amesema mamlaka hiyo imefadhili mradi huo kwa Sh bilioni 6.8, lengo likiwa ni kusaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi na kuboresha afya zao kwa kutumia nishati salama.

“Wakazi walionufaika na mradi huo ni kutoka mikoa ya Lindi na Pwani ambapo jumla ya kaya 1,000 na taasisi moja imenufaika na kurahisisha gharama za maisha pia hivi tunatarajia Shule ya Msingi Kisemvule itaingizwa katika mradi huo kwa kuwekewa jiko linalotumia mfumo huo wa gesi” amesema.

Ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2026/2027 wanatarajia kuwezesha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo utakaogharimu Sh bilioni 7.

“Kwa sasa sheria ya kuanzishwa kwa wakala ipo katika mchakato wa kufanyiwa mapitio ili kupanua wigo wa majukumu kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hizo kwa wananchi” amesema.

Amesema mradi huo ulianza Machi mwaka jana na kukamilika Januari mwaka huu, umefadhiliwa na REA na umewanufaisha kaya 530 mkoani Pwani, kaya 470 mkoani Lindi pamoja na taasisi moja.

Amesema mfumo wa matumizi ya huduma hiyo ni wa malipo kabla (prepaid), kama ilivyo Luku ambapo wananchi wamefungiwa mita, na hununua tokeni na kuingiza kwenye mita kisha kuanza kutumia.

“Gharama za Unit moja inaanzia Sh 1,000 ambapo familia ya watu sita wanaweza kutumia unit moja kwa kupika milo mitatu kwa siku hivyo inaweza ikatumika siku mbili na zaidi kutokana na matumizi ya muhusika,” amesema.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza unafuu wa gharama na urahisi wa kutumia gesi hiyo.
Mariam Rashid, mkazi wa Kisemvule amesema tangu aanze kutumia gesi hiyo ameacha matumizi ya mkaa, na gesi inapokwisha anaweza kununua muda wowote.

“Naweza kununua gesi ya Sh 1,000 ambayo natumia kwa siku tatu. Sihangaiki kama zamani. Tunaishukuru Serikali kwa kubuni mpango huu.

“Wakati watu wa REA walipokuja kuhamasisha mradi, baadhi ya wananchi walikataa kwa kuhofia nyumba zao zitalipuka, lakini sasa wanakuja kwangu niwape mawasiliano ya watu wa REA ili nao wawekewe.”

Amesema anapata unafuu hasa wakati huu wa mwezi wa Ramadhani kwani hatumii gharama kubwa kupika futari na daku.
“Zamani nilikuwa natumia vipimo vinne vya mkaa kwa siku ambavyo kila kimoja ni Sh1,000. Hata nilipokuwa natumia gesi za mitungi nilikuwa na wasiwasi wa kuisha ghafla,” amesema Mariam mwenye kaya ya watu watano.

Naye Mariam Sekena, mkazi wa Kisemvule amesema tangu aanze kutumia gesi hiyo miezi miwili iliyopita ameona nafuu kubwa katika matumizi ya nishati ya kupikia na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kitangwi kilichopo Kata ya Vikindu, Hussein Shemndolwa amesema bado wananchi wengi wanahitaji kufikiwa na huduma hiyo kwani kitongoji hicho kina kaya zaidi ya 12,000.

“REA iendelee kufadhili miradi ya aina hii ili wananchi wengi zaidi wanufaike kwa kuwa ni huduma nafuu na rahisi,” amesema