WIZARA ya Kilimo pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara zimeanza kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kuhusu marufuku ya lumbesa katika mazao ya kilimo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Machi 15, 2026 na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde katika mkutano wa hadhara wa Waziri Mkuu uliofanyika kata ya Songambele, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, mkoani Katavi.

Amesema kuwa wizara hizo zinamaliza hatua za mwisho za utekelezaji wa agizo hilo ikiwemo kupata magunia ambayo yataingia ujazo halisi unaotakiwa.“Ulituelekeza tutoke kwenye lumbesa na turudi kwenye vipimo halisi visivyozidi kilo 100 kwa kila gunia” Amesema Mheshimiwa Silinde.

Kwa nyakati tofauti akiwa katika mikutano ya hadhara aliyoifanya hivi karibuni, Mheshimiwa Dkt Mwigulu alielekeza mamlaka zinazohusika na masuala ya vipimo zihakikishe zinadhibiti  matumizi ya lumbesa kwa kuwa yanawaumiza wakulima nchini.

Akiwa katika ziara hizo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu alisema mfumo wa lumbesa ni wa kizamani na unawaumiza wakulima. “Hakikisheni katika kipindi cha mwezi mmoja sitaki kusikia habari ya Lumbesa.” alisema Waziri Waziri Mkuu akiwa Vunjo mkoani Kilimanjaro na Karatu mkoani Arusha.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewaagiza Mawaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI na Maliasili na Utalii kwenda katika Halmashauri ya wilaya ya Nsimbo na kukutana na wananchi kusikiliza kero zinazohusu sekta zao na kushirikiana nao katika kuzitatua.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ametoa hilo kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kata ya Songambele wilayani humo.

Miongoni mwa malalamiko waliyoyawasilisha ni pamoja na kukosa maeneo ya kilimo pamoja na shughuli zingine za kijamii wakidai mengi kuchukuliwa na hifadhi, kuuzwa na watendaji wa vijiji, hivyo wameiomba Serikali iwasaidie.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande ametumia fursa hiyo kumuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watahakikisha wanarudi katika eneo hilo pamoja na watendaji kwa ajili ya kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.

Vilevile, Naibu Waziri huyo ameuagiza viongozi wa Wakala wa Misitu Tanzania ( TFS ), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wasichukue hatua mkononi na badala yake wakae na wananchi na kuwaelimisha.