Na Peter Haule, WF, Arusha

Waziri wa Fedha Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa mchango wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache katika Mfuko Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina umeongezeka kutoka shilingi bilioni 58.26 mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 266.52 mwaka 2024.

Hayo yamebainishwa katika Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.

Alisema kuwa kiwango hicho kilichoongezeka ni asilimia 357 ndani ya kipindi cha miaka mitano, jambo linalopongezwa kutokana na juhudi zilizofanyika kupitia ofisi hiyo ya Msajili wa Hazina.

“Kwa sasa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache zinaunda asilimia 18 ya taasisi 308 zilizo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, huku uwekezaji wa Serikali ukiwa na thamani ya shilingi trilioni 3.6 kufikia mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo kati ya hizo shilingi trilioni 1.94 ni uwekezaji wa ndani”, alisema Mhe. Balozi Omar.

Mhe. Balozi Omar, alitoa wito kwa Mamlaka ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuendelea kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unasimamiwa kwa umakini, unazalisha faida na unachangia ukuaji wa uchumi.

Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) akieleza kuhusu mchango wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache katika Mfuko Mkuu wa Serikali wakati Mkutano wa Mwaka wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni hizo, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.

Mhe. Balozi Omar, amepongeza mageuzi yaliyotekelezwa katika Mashirika ya Umma chini ya uongozi wa Msajili wa Hazina ambapo yamechangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na utendaji kazi, jambo linalodhihirika kupitia ongezeko la kihistoria la mchango wa mapato yasiyotokana na kodi kwa Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Vilevile alisema kuwa Jukwaa la Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache limekuwa jukwaa muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kuwaleta pamoja viongozi wanaosimamia kampuni hizo.

Pia ameshukuru msaada wa washirika wa kimkakati na wadhamini ambao michango yao imewezesha kufanyika kwa jukwaa hilo, ikiwa ni pamoja na Benki ya NMB kama mdhamini mkuu wa tukio hilo, kwa dhamira endelevu ya kuunga mkono mipango ya Serikali jambo ambalo ni kielelezo cha moyo wa uzalendo kwa taifa.

Akizungumzia Dira 2050 , Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, Dira imeweka mwelekeo wa sera pamoja na ramani ya kimkakati ya maendeleo ya taifa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo, hivyo inahitaji sekta ya umma na sekta binafsi kufikiri, kufanya kazi na kusonga mbele pamoja ili kubadilisha vipaumbele vya kitaifa kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa, akieleza kuhusu umuhimu wa uwekezaji, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa wa Mwaka wa Jukwaa la Wakurugenzi wa Bodi za Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu alisema kuwa, Jukwaa hilo linatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na maarifa katika maeneo mbalimbali ya yakiwemo ya Ubunifu katika mazingira ya shinikizo la mabadiliko na Ujasusi wa kiuchumi na ushindani.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni pamoja na Kujenga uthabiti wa taasisi, kuandaa mifumo ya sekta ya madini iliyo tayari kwa siku zijazo, nafasi ya kampuni zenye uwekezaji wa hisa ndogo katika Dira 2050 na Uendelevu wa thamani ya muda mrefu.

Mkutano huo wenye kauli mbiu“Kutoka ufuatiliaji wa kawaida: Hadi Uongozi wa kimkakati unaoangaza mbele” unafanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 16 hadi 18 Machi, 2026, jijini Arusha.

Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu, akieleza fursa za Mkutano wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu , wakati wa mkutano huo unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.
Baadhi ya Wabunge na wajumbe wa mkutano wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Mwaka wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.
Jukwaa Kuu likiongozwa na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (katikati), wakati wa ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Mwaka wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiteta jambo na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Dkt. Fred Msemwa (wa pili kulia) Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu (wa pili kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji, Mhe. Masanja Kadogosa (kushoto), baada ya ufunguzi rasmi wa mkutano wa Mwaka wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha.
Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi na wajumbe wa  Mkutano wa Mwaka wa Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa Hisa Chache, unaofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), jijini Arusha. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)