Na WMMJW- New York Marekani.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, inaendelea kuimarisha hatua za kinga na huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na watoto kupitia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA–VAWC II) wa mwaka 2024/25 hadi 2028/29 pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akishiriki Mkutano wa pembeni ulioandaliwa na nchi ya Liberia uliolenga kutathmini maendeleo na changamoto katika mapambano dhidi ya ukeketaji ndani ya Mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York nchini Marekani.Waziri Dkt. Gwajima amesema, Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha juhudi za kutokomeza ukeketaji nchini huku akisema ukeketaji ni kitendo cha ukatili wa kijinsia na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wanawake na watoto wa kike.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Utafiti wa Afya na Viashiria vya Malaria wa Tanzania wa mwaka 2022 (TDHS-MIS), kiwango cha ukeketaji kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kimepungua kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 huku kukiwa bado na maeneo yenye viwango vya juu hususan mikoa ya Arusha na Manyara yenye asilimia 43 kila mmoja ikifuatia na mingine.
Akifafanua athari za ukeketaji, Waziri Dkt. Gwajima alisema kitendo hicho husababisha madhara makubwa ya kiafya na kisaikolojia, ikiwemo maumivu makali, kutokwa na damu nyingi, maambukizi ya magonjwa, matatizo wakati wa kujifungua na wakati mwingine kusababisha vifo vya Wanawake.Mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Masuala ya Jinsia wa Liberia Mhe. Gbeme Horace-Kollie huku ukihudhuriwa na Mawaziri wa masuala ya Jinsia kutoka nchi za Liberia, Kenya, Tanzania, Gambia na Wawakilishi wa Shirika la UN Women.




