▪️Ni Mradi wa Panda Hill wa Niobium utakaogharimu TSh 700 bn
▪️Ni uwekezaji unaohusisha Kampuni ya Denham ya Marekani.
▪️Rais Samia apongezwa kufanikisha mradi wa uchimbaji Niobium
▪️Kiwanda cha kuyeyusha ferroniobium kitakachojengwa Tanzania kitakuwa cha nne duniani
▪️Waziri Mavunde asema Tanzania kuchangia takriban asilimia 4 ya uzalishaji wa Niobium na uzalishaji wa takriban tani 100,000 kwa mwaka
▪️Ajira kufikia takriban watu 7,000
MBEYA, Machi 24, 2026 — Tanzania imeingia hatua muhimu ya kuimarisha biashara na Marekani baada ya Serikali na Panda Hill Tanzania Limited kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendeleza Mradi wa Niobium wa Panda Hill, hatua inayolenga kuifanya Mbeya kuwa kitovu cha uzalishaji na usindikaji wa madini mkakati.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini Mheshimiwa Anthony Mavunde alisema mradi huo ni wa uzalishaji wa madini adimu ambayo hayapatikani kila mahali duniani, na kwamba Tanzania inalenga kuchukua nafasi ya kipekee katika soko la kimataifa la niobium kupitia mradi huo.
Alisema soko la dunia kwa sasa linatawaliwa na wazalishaji wachache wakubwa, na Panda Hill itaiweka Tanzania kwenye ramani ya wazalishaji wakuu duniani.

Mheshimiwa Mavunde alieleza kuwa mzalishaji mkubwa duniani yupo Brazil na huzalisha takriban asilimia 80 ya mahitaji ya dunia, mzalishaji wa pili naye yupo Brazil na huzalisha takriban asilimia 11, huku Canada ikichangia takriban asilimia 6. Kupitia Panda Hill, alisema Tanzania inalenga kuwa mzalishaji wa nne duniani kwa kuchangia takriban asilimia 4 ya mahitaji ya dunia, na uzalishaji unaolengwa kufikia takriban tani 100,000 kwa mwaka.
Katika kusisitiza mwelekeo wa Serikali, Waziri Mavunde alisema dira ya maendeleo ya 2025-2050 na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yanalenga kuhakikisha madini yanaongezewa thamani hapa hapa nchini ili manufaa yawe makubwa kwa wananchi. Alisema Tanzania inaenda zaidi ya uchimbaji wa kawaida kwa kujenga uwezo wa ndani wa kuchakata na kuzalisha bidhaa za viwandani zenye thamani kubwa.
Mradi huo unahusisha niobium, madini ya kimkakati inayotumika kuongeza uimara wa chuma na kutengeneza aloi za utendaji wa juu zinazohitajika kwenye miundombinu mikubwa, miundombinu na matumizi ya teknolojia za kisasa. Waziri Mavunde alitaja pia matumizi katika maeneo ya kisasa kama yanayohusiana na magari ya umeme na injini za ndege, akieleza kuwa hii inaongeza uzito wa mradi katika uchumi wa kisasa wa viwanda.
Kwa upande wa mwekezaji, Dennis Cook, ambaye ni Meneja Mkuu wa Panda Hill Tanzania Limited, alisema kampuni inaingia kwenye hatua mpya ya utekelezaji kwa kushirikiana na Serikali kama mshirika rasmi, baada ya kipindi kirefu cha majadiliano na maandalizi.

Alieleza kuwa mradi ulikuwa karibu kuanza ujenzi mwaka 2017 kabla ya mabadiliko ya sheria, na tangu wakati huo kampuni imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Serikali kuhitimisha makubaliano ya msingi ya kuusukuma mradi mbele.
Cook alisema hatua zinazofuata ni kuendelea na taratibu za kupata Leseni Maalum ya Uchimbaji Madini, kusasisha taarifa za upembuzi yakinifu ili kuakisi gharama za sasa za uwekezaji na uendeshaji, kuingiza matumizi ya umeme wa gridi kwenye mpango wa uendeshaji, pamoja na kufanya tathmini ya masoko ya ferroniobium ili kuhakikisha bidhaa inaingia kwa ushindani kwenye soko la dunia, ikiwemo soko la Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa za kampuni hiyo, mradi unahusisha ujenzi wa mgodi wa niobium pamoja na kituo cha uchenjuaji na kiwanda cha kuzalisha ferroniobium, bidhaa yenye thamani iliyoongezwa inayohitajika na viwanda vya chuma na uzalishaji wa viwandani.
Kampuni imeeleza kuwa bidhaa hiyo inalengwa kuuzwa kwenye masoko ya Afrika, Asia, Ulaya na Marekani, na hivyo kuifanya Tanzania kuwa mshiriki wa moja kwa moja katika minyororo ya ugavi ya viwanda ya thamani ya juu.

Kipengele kinachoifanya Panda Hill kuwa ya kipekee, kwa mujibu wa taarifa za kampuni, ni ujenzi wa kiwanda cha ferroniobium ambacho kitakuwa cha pekee barani Afrika na kitakuwa cha nne kujengwa duniani katika kipindi cha miaka 40 iliyopita. Hili linaipa Tanzania nafasi ya kuingia kwenye kundi dogo la nchi zenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hiyo kwa kiwango cha viwandani.
Kwa biashara za ndani na wazabuni wa Tanzania, mradi umebeba fursa kubwa ya muda mrefu. Panda Hill imeeleza kuwa katika maisha ya mradi, thamani ya manunuzi ya ndani inakadiriwa kufikia Dola za Marekani bilioni 1.77, huku asilimia 70 ya manunuzi ya bidhaa na huduma ikilengwa kufanyika ndani ya nchi wakati wa uzalishaji.
Hii, kwa maelezo ya wadau, inamaanisha mikataba ya muda mrefu kwa kampuni za Kitanzania katika maeneo ya ujenzi, usafirishaji, matengenezo, huduma za kiufundi, ulinzi, chakula na huduma nyingine muhimu za uendeshaji.
Kuhusu ajira, Waziri Mavunde alisema mradi unatarajiwa kuajiri zaidi ya 1,600 kusaidia ujenzi na kutoa ajira za kudumu takriban 600, huku jumla ya watu watakaonufaika moja kwa moja na wasio wa moja kwa moja ikitarajiwa kufikia takriban 7,000.
Mradi uko katika eneo la Gereza la Kilimo la Songwe, na Waziri Mavunde alieleza kuwa takriban ekari 5,434 za eneo la mradi zipo ndani ya eneo la gereza hilo. Aliongeza kuwa mpango wa utekelezaji unahusisha ujenzi wa gereza jipya la kisasa, akieleza kuwa linalenga kuwa miongoni mwa magereza ya kisasa zaidi katika Afrika Mashariki na Kati.

Waziri Mavunde alisisitiza pia kuwa kurejesha kwa jamii ni sharti, akisema uwajibikaji wa mwekezaji kwa jamii na miradi ya kijamii ni sehemu ya lazima ya uendeshaji wa mradi, sambamba na mapato ya Serikali kupitia kodi, tozo na ushuru mbalimbali.
Kwa upande wa ushiriki wa Serikali, ilielezwa kuwa Tanzania itakuwa na umiliki wa hisa asilimia 16 kupitia mfumo wa free carried interest, unaolenga kuimarisha ushiriki wa Taifa katika maamuzi ya kimkakati na faida za mradi.
Katika hatua ya utiaji saini, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Samwel M. Maneno alisaini Framework Agreement kwa niaba ya Serikali, huku Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakisaini Shareholder Agreement na wawekezaji, kukamilisha muundo wa ushiriki wa Serikali na mfumo wa usimamizi wa mradi.







