Na Bituro Kazeri, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Biblia ni miongoni mwa vitabu vya kale zaidi vilivyowahi kusomwa na binadamu.

Ndani yake kuna hazina kubwa ya maarifa yanayoweza kumsaidia mtu kuelewa maisha, uumbaji na wajibu wa binadamu kwa mazingira yanayomzunguka.

Miongoni mwa mambo yanayojitokeza kwa uzito mkubwa ni nafasi ya ardhi katika maisha ya binadamu na viumbe wengine.

Kwa mujibu wa simulizi za Biblia, ardhi si kitu cha kawaida tu cha kukanyagwa au kutumiwa bila mipaka. Ni sehemu ya uumbaji wa Mungu, chanzo cha uhai na msingi wa maisha ya mimea, wanyama na mwanadamu mwenyewe.

Biblia inasema mwanadamu aliumbwa kwa mavumbi ya udongo na akapuliziwa pumzi ya uhai. Maana yake ni kwamba mwanadamu na ardhi vina uhusiano wa moja kwa moja usiotenganishika.

Aidha, katika maandiko hayo, Mungu anaonekana kuitambua ardhi kama chemchemi ya uzalishaji wa viumbe hai.

Nchi iliamriwa kutoa viumbe vya kila aina; wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini.

Hivyo, ardhi si tu urithi wetu, bali ni msingi wa uchumi, mamlaka, uzalishaji na ustawi wa jamii.

Lakini pamoja na umuhimu huo, Biblia pia inaweka bayana wajibu wa mwanadamu kwa ardhi. Mwanadamu hakupewa tu kuitumia, bali aliagizwa ailime na kuitunza.

Hapa ndipo swali kubwa la kizazi chetu linapoanzia: je, kweli tunaitunza ardhi kama tulivyoagizwa, au tunaimaliza taratibu huku tukijidanganya kuwa tunaendeleza kilimo?

Leo hii, ardhi inapotajwa mara nyingi ni kwa sababu ya migogoro ya viwanja, ujenzi au biashara ya pembejeo.

Haisikiki tena kama zawadi ya Mungu inayopaswa kuhifadhiwa kwa vizazi vijavyo. Tumetoka mbali na maana halisi ya agizo la kuitunza ardhi. Badala ya kuitunza, tunaichoka, tunaidhoofisha na hatimaye tunaiacha bila uhai.

Wakulima wengi, kwa mfano, wameendelea kutumia ardhi kana kwamba ni rasilimali isiyokwisha. Wamesahau kuwa ardhi nayo kama kiumbe kingine inahitaji kupumzika, kuhuishwa na kurudishiwa virutubisho vinavyoondolewa na mazao kila msimu.

Bila malezi sahihi ya kilimo, mkulima hawezi kuelewa mahitaji ya ardhi yake wala tabia ya mazao anayopanda.

Mazao kama pamba, mihogo na viazi, kwa mfano, ni miongoni mwa mazao yanayochukua virutubisho vingi ardhini. Yanapolimwa mfululizo katika eneo lilelile bila mpangilio wa kitaalamu, husababisha ardhi kupoteza uwezo wake wa kuzalisha.

Matokeo yake, shamba hubaki na udongo usio na rutuba. Hapo ndipo tunapofika mahali pa kusema: ardhi imekwisha, kilichobaki ni udongo wa kuzikia tu.

Hali hiyo tayari inaonekana kwa maeneo mengi. Ukerewe, Mibara, Nassa, Bushozi, Zanaki na Majita ni miongoni mwa maeneo ambayo wakazi wake wanakabiliwa na changamoto hiyo.

Leo, pamoja na juhudi kubwa wanazoweka mashambani, mazao wanayopata hayalingani tena na nguvu wanazotumia. Tatizo si uvivu wa mkulima, bali ni uchovu wa ardhi.

Kilicho hatari zaidi ni kwamba kupotea kwa ardhi hakuonekani tu kwa macho, bali hata tafiti zimethibitisha.

Watafiti wa udongo kutoka Chuo cha Kilimo Uyole, Mbeya, waliofanya utafiti katika vijiji 400 vya mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa na Morogoro, walibaini kuwa kati ya asilimia 60 na 70 ya ardhi ya kilimo imepoteza ubora wake.

Hii ina maana kuwa sehemu kubwa ya mashamba inayolimwa sasa haiwezi tena kuhimili uzalishaji wenye tija kama ilivyokuwa zamani.

Mazao kama mahindi, viazi, alizeti na mpunga ni miongoni mwa yaliyoathirika zaidi. Kwa kifupi, mkulima analima kwa juhudi, lakini ardhi haimsaidii tena. Hapo ndipo tunapopaswa kujiuliza kama kweli bado tunayo ardhi, au tumebakiwa na udongo mtupu usio na uhai.

Tishio hili ni kubwa zaidi kwa sababu linagusa usalama wa chakula wa taifa. Ikiwa ardhi itaendelea kuharibika, ndoto ya Tanzania kujitosheleza kwa chakula ifikapo mwaka 2030 itakuwa ngumu kufikiwa.

Zaidi ya hapo, mamilioni ya Watanzania wanaotegemea kilimo kama shughuli yao kuu ya kiuchumi wataendelea kuwa katika umaskini, si kwa sababu hawafanyi kazi, bali kwa sababu wanafanya kazi kwenye ardhi iliyokwisha.

Ripoti mbalimbali za kimataifa nazo zinaonyesha hali ni mbaya zaidi. Kwa mujibu wa BBC mtandaoni, wataalamu wanaripoti kuwa zaidi ya nusu ya ardhi inayotumika kwa kilimo duniani imezorota.

Nchini India, ambako kilimo kinakabiliwa na changamoto kubwa, uharibifu wa udongo umetajwa kuwa miongoni mwa sababu za madeni makubwa ya wakulima.

Profesa David Montgomery wa Chuo Kikuu cha Washington amenukuliwa akisisitiza umuhimu wa kupumzisha ardhi ili ipate nafasi ya kujihuisha.

Vilevile, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeripoti kuwa asilimia 33 ya ardhi ya dunia tayari imeharibiwa, na hali hiyo inaweza kufikia asilimia 90 ifikapo mwaka 2050 kama hatua za haraka hazitachukuliwa.

Hizi si takwimu za kutisha kwa bahati mbaya; ni onyo la wazi kwa dunia nzima, na kwa Tanzania pia.

Sababu za kupotea kwa ardhi na kubaki udongo wa kuzikia ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni tabia zetu wenyewe.

Kwanza, ni kushindwa kutambua kuwa ardhi ni uhai. Pili, ni kulisha mifugo kupita kiasi katika maeneo madogo. Tatu, ni kupanda zao lilelile mfululizo bila kubadilisha mfumo wa uzalishaji.

Nne, ni matumizi holela ya dawa za kuua wadudu na kemikali nyingine zinazouathiri udongo. Tano, ni matumizi ya teknolojia za kulima zinazopindua udongo kupita kiasi na kuharibu viumbe hai vilivyomo ndani yake ambavyo ndivyo msingi wa rutuba.

Ukarabati wa ardhi iliyoharibika si jambo jepesi. Unahitaji muda, maarifa, uvumilivu na gharama kubwa. Ndiyo maana njia bora si kusubiri hadi ardhi iharibike ndipo tuanze kutafuta tiba, bali ni kuzuia uharibifu huo tangu mwanzo.

Kilimo cha baadaye kinapaswa kujengwa juu ya misingi ya kuhifadhi ardhi, si kuimaliza.

Tunapaswa kurejea kwenye kilimo kinachoheshimu ardhi; kilimo kinachotambua kuwa ardhi si kiwanda cha kuzalisha mazao tu, bali ni uhai wenyewe.

Tukiendelea kuichosha, kuigeuza soko la pembejeo na kuiona kama bidhaa ya kutumia hadi iishe, tutafika mahali ambapo watoto wetu hawatarithi mashamba, bali mashimo ya udongo usiozaa.

Kwa hiyo, onyo ni hili: ardhi inapopotea, haiwi rahisi kuirudisha. Na uhai unapopotea, sayansi ya kuurudisha kwa ukamilifu bado hatuna. Hivyo, juhudi zetu zinapaswa kuelekezwa katika kulinda ardhi kabla haijageuka kabisa kuwa udongo wa kuzikia.

Mwisho wa yote, tunapaswa kukumbuka kuwa ardhi si mali yetu ya mwisho; ni amana tuliyopewa. Siku moja tutajikuta mbele ya Muumba. Swali litabaki: tulimkabidhi nini? Ardhi yenye uhai, au udongo wa kuzikia?

Mwandishi wa makala hii ni mwanachama wa Taasisi ya Wasosiolojia wa Tanzania.

0784659187; Email: [email protected]