Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mwenyekiti wa zamani wa Soka Mkoa wa Dodoma,(DOREFA) Nassoro Kipenzi ameshauri mambo matatu kwa Chama cha Soka Mkoani Dodoma ikiwemo kuhakikisha soka linachezwa wilayani.

Kipenzi ametoa kauli hiyo leo Machi 28,2026 wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (DOREFA)

Kipenzi ambaye aliiongoza Dorefa kwa miaka 8 kuanzia mwaka 2008-2016 na kumwachia Mulamu Ng’ambi ambaye aliongoza mpaka mwaka 2020 na kumwachia Mwenyekiti wa sasa Aden Mohammed.

Mwenyekiti huyo Mstaafu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo, amesema licha ya mafanikio ambayo imeyapata Dorefa inatakiwa kuendelea kusisitiza soka kuchezwa Wilayani.

“Nilienda Wilaya ya Chamwino kule nilikuta soka linachezwa sasa hii iwe kote soka lichezwe ili kutoa nafasi ya vipaji kuonekana,”amesema Kipenzi.

Pia ameshauri kuendelea kuhakikisha inazilinda klabu za Dodoma Jiji inayoshiriki Ligi Kuu na Gunners inayoshiriki Championship kuhakikisha zinaendelea kufanya vizuri.

Vilevile ameshauri kuendelea kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa kimbilio kwa klabu zingine ambazo zinautumia uwanja wa Jamhuri kama uwanja wa nyumbani.

“Dodoma imekuwa kimbilio hapa tuna Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons zinautumia kama uwanja wa nyumbani endeleeni kuzipa ushirikiano ili ziendelee kuutumia kama uwanja wa nyumbani,”amesema Kipenzi.