Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV amewataka wakaazi wa taifa tajiri la Monaco kutumia utajiri wao, ushawishi na imani yao ya Kikatoliki kutenda yaliyo mema.
Ameyasema hayo akiwa katika ziara ya siku moja nchini humo. Akizungumza baada ya kukaribishwa na Mwanamfalme Albert wa II na mkewe Charlene, Papa Leo ametoa wito kwa taifa hilo kudumisha amani na kulinda maisha ya watu na kusisitiza kuwa hakuna anayepaswa kutengwa na jamii.
Ziara ya kwanza ya Papa tangu mwaka 1538
Leo, ni Papa wa Kwanza kutembelea taifa hilo dogo lenye jumla ya watu 38,000 tangu Papa Paulo III alipofanya ziara yake mnamo mwaka 1538. Monaco ni moja ya mataifa machache ya Ulaya yanayoitambua Katoliki kama dini rasmi ya taifa.
Hivi karibuni, Mwanamfalme Albert alikataa pendekezo la kuhalalisha kuavya mimba, hatua iliyoonesha umuhimu wa imani ya Kanisa Katoliki katika jamii ya Monaco.



