Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Serikali imesema idadi ya wagonjwa kutoka nje ya nchi wanaokuja kupata huduma za matibabu nchini Tanzania imeendelea kuongezeka, ikifikia wagonjwa 3,018 katika kipindi cha miezi nane, jambo linaloashiria kukua kwa kasi kwa sekta ya utalii wa tiba.

Akizungumza bungeni Aprili 08, 2026, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi,wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dkt. Catherine Canute Joachim, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, katika Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Tatu, Kikao cha Nne amesema mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya.

Dkt. Samizi amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza nguvu katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya hospitali, hatua iliyochangia kuimarika kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Ameongeza kuwa pamoja na miundombinu, Serikali imewekeza katika ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa ikiwemo PET/CT Scan, Angio Suite, Cathlab na CT Scan, huku ikiendelea kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa afya kupitia mafunzo maalum.

“Tunapanua huduma za ubingwa bobezi na kuhakikisha hospitali zetu zinapata ithibati za kimataifa, pamoja na kuzitangaza kimataifa ili kuvutia wagonjwa zaidi kutoka nje,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, wagonjwa hao walihudumiwa katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda, maalum na taifa kati ya Julai 2025 hadi Februari 2026.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika rasilimali watu kupitia Programu ya Samia Health Super-specialization, ambapo wataalamu 1,483 wanafadhiliwa kusomea ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi.

Hatua hizi zinaendelea kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha huduma za tiba kwa wageni barani Afrika.