Wizara ya Madini imeiomba Bunge kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 174.98 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake muhimu ya kusimamia na kuendeleza sekta ya madini nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi bungeni jijini Dodoma leo Aprili 27, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema bajeti hiyo imelenga kuimarisha ufanisi wa shughuli za wizara pamoja na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa maelezo ya waziri huyo, kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 71.51 sawa na asilimia 40.87 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuendeleza miundombinu na kuongeza tija katika sekta hiyo.

Aidha, shilingi bilioni 103.47 sawa na asilimia 59.13 zitatumika kwa matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 27.36 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi, huku shilingi bilioni 76.11 zikienda katika matumizi mengine ya kiutendaji na uendeshaji wa shughuli za kila siku.

Mavunde amesisitiza kuwa utekelezaji makini wa bajeti hiyo utasaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali, ambayo yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni 1.4, sambamba na kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali madini nchini.

Bajeti hiyo inaelezwa kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa serikali wa kuifanya sekta ya madini kuwa moja ya nguzo kuu za ukuaji wa uchumi na chanzo kikubwa cha mapato ya taifa.