Na. Josephine Majura, WF, Dodoma

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha huduma za miamala ya fedha kwa mitandao ya simu zinapatikana kwa gharama nafuu, kwa kupunguza gharama za miamala ya kielektroniki, kuimarisha miundombinu ya mifumo ya malipo na kuweka mazingira rafiki ya kisera na kikanuni ili kuchochea matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali na kupunguza gharama kwa wananchi.

Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Mhe. Tarimba Gulam Abbas, ambaye alitaka kujua sababu za Serikali za kutokutoa bei elekezi kwa makato ya huduma za Mobile Money ili kuwapunguzia gharama Wananchi.

Alitaja hatua zilizochukuliwa kwa kipindi cha mwaka 2024 na 2025 ambapo katika mwaka 2024 Benki Kuu ya Tanzania iliweka kikomo cha juu cha gharama ya muamala kwa mfumo wa malipo ya papo kwa papo na mfumo wa Tanzania Automated Clearing House (TACH), ambapo gharama ya juu kwa muamala mmoja ni shilingi 2,000.

Aliongeza kuwa katika mwaka 2025, Benki Kuu ya Tanzania ilipunguza gharama za miamala ya kutuma fedha kidijitali, ikiwemo kuhamisha fedha kutoka simu kwenda akaunti za benki na kutoka benki kwenda simu kupitia mfumo wa Tanzania Instant Payment System (TIPS).

Mhe. Balozi Omar, alieleza kuwa gharama za miamala zimepunguzwa na kuwekwa ukomo wa Shilingi 5,000 kwa miamala inayozidi Shilingi 500,000, huku kwa miamala isiyozidi kiwango hicho mwongozo wa ukomo wa gharama kwa viwango tofauti ukiainishwa.

“Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali ili kuhakikisha ushindani katika sekta ya mifumo ya malipo ya kielektroniki. Hadi kufikia Machi 2026, jumla ya watoa huduma 113 walikuwa wameshapata leseni ya kutoa huduma za mifumo ya malipo nchini,” alifafanua Mheshimiwa Balozi Omar.

Aidha, alibanisha kuwa Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikiana na watoa huduma wa mifumo ya malipo ya kielektroniki kufanya tathmini ya gharama za miamala na kuchukua hatua zinazofaa za kupunguza gharama zaidi bila kuathiri uthabiti na usalama wa mfumo wa malipo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Mhe. Tarimba Gulam Abbas (hayupo pichani), ambaye alitaka kujua sababu za Serikali za kutokutoa bei elekezi kwa makato ya huduma za Mobile Money ili kuwapunguzia gharama Wananchi.