Timu ya Mpira wa Miguu ya Mashtaka imeshindwa kuonesha ubabe wake baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-2 kutoka kwa TCDC Sports Club katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Venite, Mji Mwema mkoani Njombe.
Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, TCDC Sports Club ilianza kwa kasi na kuonyesha kiwango bora tangu dakika za mwanzo. Kipindi cha kwanza kilishuhudia TCDC ikienda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, huku Mashtaka wakijitahidi kusawazisha bila mafanikio makubwa.
Kipindi cha pili kiliendelea kuwa na ushindani mkali, lakini TCDC waliendelea kutawala mchezo kwa kuongeza mabao mawili zaidi, wakionyesha umakini mkubwa katika safu yao ya ushambuliaji.
Mashtaka walifanikiwa kupata bao moja la kufutia machozi, lakini halikutosha kuzuia ushindi wa TCDC, na hivyo mchezo kumalizika kwa mabao 4-2.
Ushindi huo unaipa TCDC Sports Club morali kubwa wanapoendelea na maandalizi yao kupitia mechi za kirafiki dhidi ya timu mbalimbali za Wizara na Taasisi.
Mechi hizo ni sehemu ya kujiandaa kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka 2026, yatakayofanyika kitaifa mkoani Njombe.
Kwa upande wao, Mashtaka watalazimika kujipanga upya na kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ili kuimarisha kikosi chao katika michezo ijayo.




