Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeweka wazi vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuimarisha miundombinu ya sekta, kukamilisha maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027 pamoja na kukuza Kiswahili kimataifa.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo leo Mei 4,2026 Dodoma, Waziri wa wizara hiyo Paul Makonda amezungumzia maandalizi ya AFCON 2027 kwama serikali inaendelea kukamilisha miundombinu ya michezo na kuunganisha wadau mbalimbali wa sekta za utalii, usafiri, malazi na burudani ili kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na mashindano hayo.
Aidha amesema Serikali itajikita pia katika kuandaa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia ya urembo (Miss World), pamoja na kuboresha sera, sheria na miongozo ya sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo.
Amesema vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi, kukuza vipaji vya michezo, kuboresha mafunzo ya sanaa na utamaduni, pamoja na kuratibu matamasha na matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa.
Makonda amebainisha kuwa wizara hiyo itaendelea kuimarisha upatikanaji wa maudhui kupitia vyombo vya habari vya umma ikiwemo Tanzania Broadcasting Corporation (TBC), sambamba na kuongeza usimamizi wa maadili ya uandishi wa habari na utoaji wa elimu kwa wadau wa sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, amesema serikali imejipanga kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 20 kwa wadau zaidi ya 8,000 wa tasnia ya habari, utamaduni na sanaa, hatua inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 100,000 kwa vijana.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinafanyika chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya michezo na utamaduni ili kukuza uchumi wa nchi.
Awali akiwasilisha hotuba hiyo, Makonda ameomba Bunge lipokee, lijadili na kupitisha makadirio ya wizara (Fungu 96) kwa mwaka wa fedha 2026/27, akieleza kuwa sekta anazosimamia zina mchango mkubwa katika ajira, utambulisho wa taifa na maendeleo ya uchumi.




