Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naandika makala hii nikiwa safarini kuelekea Kilimanjaro, kushiriki mazishi ya Baba Mzazi wa Ndugu yetu, kijana na rafiki yetu, Neville Meena, mzee Mwalimu Meena. Baba huyu ametutoka na Mungu amlaze mahala pema peponi. Kichwa cha kama hii kinahanikiza maridhiano. Maridhiano haya yanayoguswa ni ya ndani ya vyama na nje ya vyama vya siasa.

Sitanii, kuna wakati taifa linafika mahali ambapo hasira, majonzi na lawama vinakuwa vingi kuliko maneno ya matumaini. Ndivyo ilivyo kwa Tanzania baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025 yaliyoacha simanzi kubwa, machozi na vifo vya watu 518. Hili si jambo dogo. Ni jeraha kubwa katika historia yetu. Lakini katika nyakati kama hizi ndipo busara ya taifa hupimwa.

Tanzania imejengwa juu ya msingi wa maridhiano, uvumilivu na kuheshimiana. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kutukumbusha kuwa taifa linaweza kujengwa kwa umoja, lakini haliwezi kujengwa kwa chuki. Leo tunapaswa kujiuliza; tunataka kuendelekea njia ya visasi au turudi katika njia ya maridhiano?

Ni kweli, maumivu yaliyotokea hayawezi kufutwa kwa maneno matamu. Familia zilizopoteza ndugu zao zina huzuni halali. Wapo waliojeruhiwa, waliopoteza mali zao na waliobeba majeraha ya kisaikolojia. Lakini tukikubali hasira zitawale, tutajikuta tunajenga taifa la mashaka, hofu na migawanyiko ya kudumu.

Ndiyo maana jitihada za maridhiano zinapaswa kupewa nafasi. Mazungumzo si udhaifu. Kusikilizana si usaliti. Na kutafuta suluhu si kuhalalisha makosa yaliyotokea. Taifa lolote lenye busara hujifunza kwamba baada ya migogoro mikubwa, kinachofuata lazima kiwe mazungumzo ya kweli na haki ya kweli.

Tusidanganywe na wale wanaotaka Watanzania waishi katika hasira za milele. Wapo wanaonufaika kisiasa na machafuko. Wapo wanaoamini kuwa taifa likigawanyika wao hupata nguvu zaidi. Lakini historia ya dunia inaonyesha kuwa nchi nyingi zilizoingia katika siasa za kulipizana kisasi ziliingia pia katika miaka mingi ya vurugu na umasikini.

Sitanii, leo Tanzania inahitaji moyo wa kuponya taifa. Tunahitaji viongozi wa dini, wazee wa kimila, wasomi, wanahabari na wanasiasa kukaa pamoja na kujenga daraja la matumaini. Hatuwezi kujenga Dira ya Taifa ya 2050 huku mioyo ya watu ikiwa imejaa hofu na majeraha ya kisiasa.

Maridhiano hayamaanishi kuficha ukweli. Hapana. Ukweli lazima ujulikane. Uchunguzi wa haki ufanyike. Waliobeba dhamana ya uongozi wawajibike pale inapobidi. Lakini haki hiyo ifanywe kwa hekima, si kwa jazba. Taifa lisigeuzwe uwanja wa kulipizana visasi.

Watanzania wengi wanataka amani. Wanataka kuona watoto wao wakisoma kwa utulivu, biashara zikifanyika na nchi ikisonga mbele. Wananchi hawataki kusikia vilio vya chuki kila siku. Wanataka kuona viongozi wakizungumza lugha ya matumaini.

Sitanii, tusiyasahau yaliyotokea, lakini tusiiache njia ya maridhiano. Tusiwape nafasi wanaotaka kutuvuruga kwa kutumia maumivu ya wananchi. Tanzania imepitia nyakati nyingi ngumu, lakini imesimama kwa sababu watu wake wanaamini katika umoja kuliko tofauti zao. Naamini yote yatapita, ila lazima tuzungumze kama Watanzania na tusidanganyane, tutoe ya moyoni. Baada ya machozi ya Oktoba 29, 2025, historia itatuhukumu kwa jambo moja kubwa; je, tulichagua kulipiza kisasi au tulichagua kujenga taifa upya? Mimi naamini bado tuna nafasi ya kuchagua njia sahihi. Njia ya maridhiano, haki na mshikamano wa kitaifa. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827