Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Songea

Wananchi wa Wilaya za Namtumbo, Songea na Mbinga mkoani Ruvuma wameishukuru idara ya Caritas ya Jimbo Kuu Katoliki la Songea kwa mchango mkubwa wa kuwainua kiuchumi kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, katika maadhimisho ya Jubeiei ya miaka 50 tangu kuanzisha kwa Idara hiyo ya utume wa Caritas Jana katika uwanja wa michezo wa Majimaji uliopo Manispaa ya Songea,wananchi hao wamesema kuwa kupitia programu zinazoratibiwa na Caritas, wameweza kupata mafunzo ya ujasiriamali, mikopo midogo, elimu ya kilimo bora pamoja na ufugaji wa kisasa jambo ambalo limechangia kuongeza kipato cha familia zao na kuboresha maisha kwa ujumla.

Zuberi Juma mkulima wa zao la Soya kutoka Wilaya ya Namtumbo amesema kuwa kabla ya kujiunga na vikundi vya kiuchumi vilivyowezeshwa na Caritas, alikuwa anakabiliwa na changamoto za kipato na uzalishaji mdogo wa mazao. Hata hivyo, kwa sasa ameweza kupanua shughuli zake za uzalishaji na kujitegemea kifedha.

Naye mkazi wa Wilaya ya Mbinga Singirada Matembo amesema kuwa msaada unaotolewa na Caritas umeongeza mshikamano katika jamii kupitia vikundi vya kuweka na kukopa, hali iliyowasaidia wanawake na vijana wengi kuanzisha biashara ndogondogo na kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa utume wa Caritas katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea Jojina Mbawala amesema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kusaidia jamii zenye changamoto za kimaisha kujitegemea kwa kuwapatia wananchi maarifa na fursa za maendeleo endelevu.

Amesema Caritas itaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha jamii nyingi zaidi zinanufaika na programu hizo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Naye mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la madaba na mwenyekiti wa bunge 2020/2025 Joseph Mhagama ameitaka jamii kuendelea kutumia vizuri fursa zinazotolewa na utume wa Caritas katika kuleta maendeleo ya mtu Mmoja Mmoja na Taifa kwa ujumla.