BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) imesema imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), ikieleza kuwa kasi ya ujenzi ni dalili njema ya kuanza kwa usafirishaji wa mafuta ndani ya muda uliopangwa.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Ngosi Mwihava amesema wakati akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa bodi hiyo waliotembelea sehemu ya mradi katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera kwa lengo la kujionea maendeleo na utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati unaounganisha Uganda na Tanzania.

Bw.Mwihava amesema bodi hiyo imevutiwa na namna mkandarasi anavyotekeleza mradi huo kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, ratiba ya utekelezaji pamoja na masharti ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya jamii zinazozunguka mradi.

“ Ewura ndiyo imetoa kibali cha ujenzi wa bomba hili kwa upande wa Tanzania na ziara hii, ambayo ilianzia Dodoma ina lengo la kuhakikisha yale yote tuliyokubaliana , ikiwemo utunzaji wa mazingira, kutoa kipaumbele cha ajira kwa Watanzania na maeneo mengine yatatekelezwa,”

“Ewura pia itahusika kutoa vibali pia vya kuanza kazi ya usafirishaji mafuta ghafi kupitia Tanzania, pindi ujenzi wa miundombinu utakapojamilika, hivyo tumeona ni vema kufanya kazi hiyo wakati mradi huu ukiendelea ukingoni,” amesema.

“Tumeshuhudia kazi kubwa ikiendelea kwa kasi ya kuridhisha. Maendeleo haya yanaonyesha kuwa matarajio ya kuona mafuta yakianza kusafirishwa kupitia bomba hili yanaweza kufikiwa ndani ya muda uliopangwa,” amesema Mwihava.

Kiujumla, mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70, huku kasi ya utekelezaji ikiendelea kwa kasi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Chongoleani mkoani Tanga ambapo ujenzi wa matenki ya kuhifadhia mafuta ukiwa umekamilika na majaribio yakifanyika.

Katika eneo hilo Pwani ya Chongoleani pia kuna ujenzi wa gati inayoelekea baharini kwa ajili ya kusafirisha mafuta kwenda nje ya nchi pindi mradi utakapoanza kazi.

Ziara hiyo ni miongoni mwa ziara mbalimbali zinazofanywa na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kuhakiki kazi zinaendelea ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Akiongea zaidi wakati wa ziara hiyo, Bw. Mwihava amesema pamoja na umuhimu wa mradi huo katika sekta ya nishati, utekelezaji wake umeendelea kuleta manufaa kwa wananchi kupitia ajira, huduma za kijamii na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wazawa katika maeneo yanayopitiwa na bomba hilo.

“Tumefurahishwa kuona kuwa masuala ya mazingira yanazingatiwa kwa umakini mkubwa. Aidha, jamii zinazozunguka mradi zimeendelea kushirikishwa na kunufaika kupitia miradi ya kijamii pamoja na ajira zinazotokana na utekelezaji wa mradi,” ameongeza.

Hata hivyo, Bw.Mwihava amemtaka mkandarasi pamoja na kampuni zinazoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo kuendelea kuzingatia kikamilifu masharti yaliyowekwa na mamlaka za usimamizi, hususan katika kuongeza ushiriki wa wazawa katika shughuli mbalimbali za mradi.

Amesisitiza kuwa Serikali ina matarajio makubwa kuona Watanzania wengi zaidi wakipata ajira, mafunzo ya ujuzi na fursa za biashara kupitia mradi huo ambao unatajwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ni muhimu kuona wazawa wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huu, siyo tu katika ajira za kawaida bali pia katika huduma za kitaalamu, usambazaji wa bidhaa na utoaji wa huduma mbalimbali zinazohitajika,” amesema.

Amesema kazi zinaendelea katika maeneo mbalimbali kwa kuzingatia viwango vya usalama, afya na mazingira, huku akibainisha kuwa ushirikiano kati ya serikali, wakandarasi na wananchi umechangia maendeleo mazuri ya mradi.

Amesema mradi huo umeendelea kutoa ajira kwa mamia ya wananchi wa maeneo yanayouzunguka, huku pia ukichochea shughuli za kiuchumi katika sekta za usafirishaji, biashara ndogo ndogo na huduma za malazi.

Mradi wa EACOP unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1,443 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo sehemu kubwa ya bomba hilo inapita nchini Tanzania.

Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya nishati Afrika Mashariki, ukiwa na matarajio ya kuongeza mapato ya serikali, kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu muhimu cha usafirishaji wa nishati katika ukanda huo.

Mradi huo unamilikiwa na kampuni ya TotalEnergies kwa asilimia 62, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Mafuta la Uganda (UNOC) kila moja likimiliki asilimia 15, na kampuni ya CNOOC ya China ikimiliki asilimia 8.