Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Viongozi wametakiwa kubadilika kulingana na teknolojia ya sasa na kuacha kuwa kiongozi anayeshangaa mabadiliko ili kuendana na kasi ya ulimwengu kwa kuchochea ubunifu na uvumbuzi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkufunzi, Padri John Kasembo leo Mei 21, 2026 akiwa anatoa mafunzo kwa wauguzi ikiwa ni siku ya pili ya Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wauguzi Viongozi unaoganyika mkoani Dodoma.
“Tuwe watu wenye uwezo wa kufanya maamuzi mazuri yenye busara, yenye kiwango kidogo cha makosa na kuwatumikiwa watu kwa kujishusha pamoja na kujali maslahi ya Taifa na ulinzi wa Taifa letu,” amesema Padri Kasembo
Padri Kasembo amewamehimizwa viongozi hao kuendelea kuwa wazalendo kwa Serikali iliyopo Madarakani kwa kutii na kutunza siri zote za Serikali kwa mujibu wa miongozo ya utumishi wa umma.
“Sisi kama watumishi tunatakiwa kuepuka kuendeleza majungu sehemu ya kazi na kuwa watu wa mfano katika katika kuonesha uzalendo kwa nchi yetu ya Tanzania pamoja na kuwaheshimu viongozi waliopewa dhamana,” amesema Padri Kasembo
Pia, Padri Kasembo amesisitiza kuwa kuwa kiongozi bora na wa kuingwa kwa kuwa uongozi ni baraka, uongozi ni mshumaa na kazi yake kutoa mwanga, uongozi ni kujitoa sadaka kwa maslahi mapana ya taasisi husika.
Mkutano huo unaowakutanisha wauguzi viongozi wa mikoa, halmashauri, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za kanda, hospitali za taifa pamoja na waratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto una lengo kubwa la kufanya tathmini ya huduma za afya katika vituo, kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma pamoja na kubadilishana uzoefu.












