Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga imemhukumu Isa Musini Rashidi maarufu kama Hamidu kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusafirisha kilo 75.15 za dawa za kulevya aina ya mirungi (Khat).
Hukumu hiyo imetolewa Julai 22, 2026 na Hakimu Mkazi Azizi M. Khamis, baada ya Mahakama kuridhika kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote ya msingi.
Katika kesi hiyo, Mahakama ilielezwa kuwa Aprili 10, 2026, katika eneo la Kinyatu ‘A’, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) walimkamata Isa akiwa anaendesha pikipiki nyeusi aina ya Huoniao yenye namba za usajili MC 569 EYG, akiwa amebeba mifuko miwili iliyokuwa na jumla ya mafungu 122 ya majani yaliyodhaniwa kuwa mirungi.
Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali ulithibitisha kuwa majani hayo yalikuwa mirungi yenye uzito wa kilo 75.15.
Katika kuthibitisha shtaka, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano na vielelezo 10, huku mshtakiwa akikana tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Baada ya kuchambua ushahidi uliowasilishwa na pande zote, Mahakama iliridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa thabiti na uliweza kuthibitisha kuwa mshtakiwa alikamatwa akiwa anasafirisha mirungi hiyo.
Mahakama pia iliridhika kuwa vielelezo vilihifadhiwa na kushughulikiwa kwa kufuata taratibu, kuanzia wakati wa ukamataji, uchunguzi wa kitaalamu hadi kuharibiwa kwa mujibu wa amri ya Mahakama.
Kwa msingi huo, Mahakama ilimtia hatiani Isa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha Kifungu cha 16(1) na (2)(c) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, Marejeo ya Mwaka 2023, na kumhukumu kifungo cha miaka 30 jela.
Aidha, Mahakama imeamuru pikipiki aina ya Huoniao yenye namba za usajili MC 569 EYG, iliyotumika kusafirisha dawa hizo, itaifishwe na kuuzwa kwa mnada wa hadhara.


