Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya kupitia mifumo imara, madhubuti na endelevu, badala ya kutegemea miradi na programu za muda mfupi.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 27 Julai 2026, alipokutana na ujumbe wa Serikali ya Uswisi ulioongozwa na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Amesema Serikali imeweka mkazo katika kujenga taasisi zenye uwezo na mifumo madhubuti itakayokidhi mahitaji ya sekta ya afya kwa muda mrefu, akibainisha kuwa kutegemea miradi ya muda mfupi pekee hakutoshi kuleta uendelevu wa huduma bora kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema mafanikio ya sekta hiyo yanategemea kuwepo kwa taasisi imara, watumishi wenye uwezo, mifumo madhubuti ya usimamizi na vyanzo vya uhakika vya fedha vitakavyowezesha huduma kutolewa kwa ufanisi wakati wote.

Aidha, amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya, ili kuongeza uwezo wa sekta hiyo kutoa huduma bora na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni hatua muhimu katika kujenga mfumo endelevu, utakaowawezesha wananchi kupata huduma wanazohitaji bila kukabiliwa na vikwazo vikubwa vya kifedha.

Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Uswisi kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika sekta ya afya, hususan katika utafiti, mapambano dhidi ya malaria na uimarishaji wa mifumo ya ugharamiaji na utoaji wa huduma za afya.

Amesema ushirikiano huo umechangia kuimarisha uwezo wa taasisi za afya na kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema ushirikiano huo umechangia kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuboresha ustawi wa wananchi, huku akisisitiza dhamira ya Zanzibar ya kuendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Uswisi katika maeneo yenye vipaumbele vya pamoja.

Kwa upande wake, Mhe. Nicole Providoli amesema Uswisi na Zanzibar zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya kuaminiana, kuheshimiana na dhamira ya pamoja ya kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi.

Amesema sekta ya afya itaendelea kuwa miongoni mwa maeneo ya kipaumbele katika ushirikiano baina ya Uswisi na Zanzibar, hususan katika kuimarisha mifumo ya afya, utafiti, ugharamiaji wa huduma na juhudi za kutokomeza malaria.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akisalimiana na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, alipofika Ikulu Zanzibar akiwa ameambatana na ujumbe wa Serikali ya Uswisi kwa ajili ya mazungumzo, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na ujumbe wa Serikali ya Uswisi ulioongozwa na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, walipofika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo, yaliofanyika leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, alipowasili Ikulu Zanzibar akiwa ameambatana na ujumbe wa Serikali ya Uswisi, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akikabidhiwa zawadi ya kitabu na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, alipowasili Ikulu Zanzibar akiwa ameambatana na ujumbe wa Serikali ya Uswisi walipofika ikulu kwa ajili ya mazungumzo, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania na Burundi, Mhe. Nicole Providoli, pamoja na ujumbe wake alioambatana nao wa Serikali ya Uswisi walipofika ikulu, leo katika Ukumbi wa Ikulu Zanzibar, tarehe 27 Julai, 2026.