Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Wizara ya Viwanda na Biashara imeeleza kuendelea kwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini kupitia operesheni maalum zinazoendeshwa na Tume ya Ushindani (FCC), ambapo hadi Aprili 2026 jumla ya chupa 4,251 za pombe bandia zimekamatwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza bungeni Mei 22, 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema operesheni hizo pia zilifanikiwa kukamata chupa tupu 286 pamoja na katoni 250 zilizokuwa zikitumika katika shughuli za ufungashaji wa bidhaa hizo bandia.

Aidha, amesema katika msako huo pia vifaa mbalimbali vilivyokuwa vinatumika katika uzalishaji wa pombe hizo bandia vilikamatwa, vikiwemo mashine za kuchapisha lebo za bidhaa, kipima kilevi, mashine za kufungia vifuniko, mizani, ethanoli pamoja na vifaa vya kuchanganyia na kuchuja pombe.

Kapinga alibainisha kuwa juhudi hizo hazijaishia kwenye pombe bandia pekee, bali FCC pia imebaini uwepo wa bidhaa nyingine bandia ikiwemo vipuri na vilainishi, ambapo hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya watuhumiwa wanaohusika.

Amesema Serikali imeweka mkazo katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia kupitia kuimarisha ufuatiliaji wa taarifa za kiintelijensia, kufanya operesheni za ukaguzi na ukamataji, pamoja na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu.