Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imeendelea kuimarisha sekta ya viwanda nchini huku Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) likisajili jumla ya viwanda 25,650 na kuongeza nguvu katika huduma za maabara pamoja na teknolojia za uzalishaji zinazolenga kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.
Akizungumza Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema TIRDO imeendelea kufanya tathmini ya viwanda na kubaini maeneo yenye fursa mpya za uwekezaji nchini.
Amesema tathmini hiyo inalenga kubaini idadi ya viwanda, ajira, uwezo wa uzalishaji pamoja na teknolojia zinazotumika ili kusaidia kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, tathmini hiyo sasa imefanyika katika mikoa tisa ambayo ni Pwani Region, Morogoro Region, Dar es Salaam, Kilimanjaro Region, Tanga Region, Arusha Region, Manyara Region, Mwanza Region na Shinyanga Region.
Amesema taarifa zote zilizokusanywa zimehifadhiwa katika mfumo wa kanzidata za viwanda ambapo hadi Aprili 2026 jumla ya viwanda 25,650 vilikuwa vimesajiliwa nchini.
“Kati ya hivyo, viwanda 482 ni vikubwa, 625 vya kati, 8,980 ni vidogo huku 15,563 vikiwa viwanda vidogo sana,” amesema Kapinga.
Katika hatua nyingine, amesema TIRDO imeendelea kuboresha maabara zake ili kuongeza ubora wa huduma za utafiti na uchunguzi wa viwanda nchini.
Ameeleza kuwa maabara ya chakula iliyopata ithibati mwaka 2025 sasa imeongeza huduma zake kutoka tatu hadi sita huku ikiongeza wigo wa bidhaa zinazopimwa kutoka moja hadi nne.
Bidhaa hizo ni pamoja na vyakula vilivyotayari kwa matumizi, nyama na bidhaa zake, samaki pamoja na sampuli za usufi wa nyuso.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, maboresho hayo yatasaidia kuongeza huduma za uhakika na kupunguza utegemezi wa huduma za maabara kutoka nje ya nchi.
Aidha, amesema TIRDO inaendelea na ujenzi wa Maabara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe Region kwa lengo la kusogeza huduma karibu na maeneo ya uzalishaji na rasilimali za madini.
Amesema maabara hiyo itahudumia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Ruvuma Region, Mbeya Region na Rukwa Region kwa kufanya vipimo vya makaa ya mawe, kemikali, madini pamoja na nishati mbadala ikiwemo biomasi na mkaa mbadala.
“Hadi Aprili 2026, tayari tumempata mzabuni wa kusambaza na kusimika vifaa vya kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaoendesha maabara hiyo,” amesema Kapinga.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa maabara hiyo kutasaidia kuchochea uchumi wa viwanda unaozingatia matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira.
Sambamba na hilo, amesema TIRDO inaendelea na mchakato wa kupata ithibati kwa maabara zake za mazingira, kemia, makaa ya mawe, mafuta na gesi ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wadau wa viwanda.
Katika eneo la ubunifu na teknolojia, Waziri Kapinga amesema Serikali kupitia Small Industries Development Organization (SIDO) imefanikiwa kuhawilisha teknolojia nane za uchakataji wa mazao na uzalishaji.
Teknolojia hizo zinajumuisha mashine za kutengeneza mkaa mbadala, kusafisha mafuta ya alizeti, kuzalisha chakula cha samaki, kubangua korosho, kukamua mafuta ya nazi pamoja na mashine za kusaga mawe yenye madini.
Aidha, amesema SIDO kwa kushirikiana na United Nations Industrial Development Organization imezalisha mashine tatu za mkaa mbadala na kuanzisha teknolojia mpya kutoka Japan katika maeneo ya Ifakara, Kahama na Mwanjelwa.



