Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo,amedai kuwa chama hicho kimepata taarifa zinazoonyesha kuwapo kwa vikao vya siri vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA kwa lengo la kuhamasisha maandamano na vurugu.
Kutokana na hali hiyo amewataka watanzania kutoruhusu makundi yoyote kuvuruga amani na utulivu wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 13,2026 Kihongosi amesema taarifa hizo zinaashiria kuwa baadhi ya wanasiasa pamoja na makundi ya wanaharakati wamekuwa wakiratibu ajenda za maandamano badala ya kushiriki katika mijadala ya maendeleo.
Amewataja viongozi wa CHADEMA akiwemo John Heche, Boniface Jacob na Godbless Lema, akiwataka kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa taifa kwa hoja na kushindana kwa sera badala ya kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
“Tunawataka wenzetu waache siasa za matukio na waingie kwenye mjadala wa kujenga nchi. Watanzania wanahitaji suluhisho la changamoto zao za kila siku, si mazingira ya taharuki na migogoro,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi, wazalendo na wapenda maendeleo kutoshabikia maandamano na vurugu kwa namna yoyote ile, akisema matukio hayo mara nyingi huwaathiri wananchi wa kawaida zaidi kuliko viongozi wa kisiasa.
“Hasara za maandamano huwa zinawakumba watu wa chini wafanyabiashara wadogo, mama lishe, bodaboda na vijana wanaojitafutia kipato,mara nyingi huwezi kuona watoto wa viongozi wa kisiasa wakipata madhara hayo ndiyo maana tunasisitiza Tanzania ijengwe kwa hoja na si kwa vurugu,” amesema.
Kihongosi ametumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania kutokubali mtego wa kubaguana kwa misingi ya kisiasa, kikabila au tofauti nyingine, akieleza kuwa umoja wa kitaifa ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na kwamba tofauti za kimtazamo zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na kuheshimiana.
Licha ya hayo amesisitiza kuwa CCM itaendelea kujikita katika kutatua changamoto za wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo afya, maji, elimu na miundombinu, akisema hicho ndicho chama kinachokipa kipaumbele.
Sambamba na hilo, ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho dhidi ya viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, huku akiwataka wananchi kushirikiana navyo kwa kutoa taarifa mapema ili kudumisha usalama wa nchi.
Akizungumzia Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, Kihongosi amesema imeonyesha hatua kubwa ya kujitegemea kiuchumi na kifedha, akitoa pongezi kwa Serikali na Bunge kwa kusimamia sera na mipango inayochochea maendeleo ya taifa.

