Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Katika siasa kuna wakati taifa linapaswa kujua tofauti kati ya kutafuta haki na kutafuta suluhu. Wakati mwingine njia ya mahakama ni muhimu pale panapokuwa na tuhuma za uhalifu, lakini pia kuna nyakati ambapo busara ya kisiasa, mazungumzo na maridhiano vinaweza kuzuia taifa kuingia kwenye mgawanyiko usio na mwisho.
Sitanii, kwa hali ya Tanzania ya sasa, kuna kila ishara yale mapendekezo ya Kikosi Kazi cha Hali ya Siasa kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kikaongozwa na Prof. Rwekaza Mukandala, yanaweza kuwa msingi wa kuanza mchakato wa maridhiano bila kusubiri kila kitu kiingie.
Najua kuna uchunguzi wa jinai unaendelea chini ya Jaji Shabani Ally Lila. Ni mchakato sahihi, ni mchakato wa kisheria zaidi kwani utabainisha uhusika wa kila awaye katika matokeo ya vurugu za Oktoba 29, 2025.
Tume ya jinai ina nafasi yake. Kama kuna makosa ya jinai, sheria lazima ifanye kazi. Lakini historia ya dunia inaonyesha kuwa mahakama mara nyingi huleta matokeo ya kisheria zaidi kuliko suluhu ya kisiasa. Mahakamani kuna mshindi na mshindwa. Kuna upande unaoshinda na mwingine unaopoteza. Lakini katika siasa, hasa siasa za ushindani, kinachotafutwa zaidi ni namna ya kujenga daraja la kuishi pamoja baada ya tofauti.
Siasa si vita ya kuangamizana. Wanasiasa wanaweza kuwa wapinzani leo, lakini kesho wakawa washirika katika kujenga taifa moja. Hapa sitaki kukumbushia Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Paschal Katambi, akina Profesa Kitila Mkumbo na wengine kuwa walikuwa CHADEMA ila leo wako CCM na serikalini wanajenga nchi kwa kasi na uadilifu wa hali ya juu. Siasa si uhasama, ni ushindani wa hoja.
Sitanii, ni kwa muktadha huo ndiyo maana nimelisema mara kadhaa na kwa uwazi suala la kumwachia Tundu Lissu. Nimesema na narudia, maana najua wapo washauri wa kutosha serikalini na wanaoaminika, hivyo kwa kusema hivi wanawaza mara mbili. Kwa masilahi mapana ya taifa letu, nasema suala hili linapaswa kutazamwa ndani ya picha kubwa ya maridhiano ya kitaifa. Taifa lenye demokrasia imara linahitaji wapinzani wake wawe na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika siasa, kutoa hoja na kushindana kwa sera.
Nisikilize vizuri. Sambamba na Lissu kuachiwa, maridhiano yanahitaji wajibu wa pande zote. Uhuru wa kisiasa unakwenda na uwajibikaji wa kauli. Ni muhimu viongozi wa kisiasa kuhakikisha lugha wanazotumia zinajenga taifa badala ya kuongeza majeraha. Mpinzani anaweza kuikosoa serikali, chama au sera bila kuvuka mipaka ya heshima kwa taasisi na watu binafsi.
Historia ya siasa za Tanzania inaonyesha kuwa hata ndani ya vyama, ushindani unapokuwa mkali unaweza kuacha makovu. Wakati wa harakati za uongozi ndani ya CHADEMA, Lissu aliwahi kumshambulia aliyekuwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kwa tuhuma nzito, ikiwamo kumtaja kama mla rushwa mkubwa. Hili linaonyesha kuwa siasa zinaweza kuwa na misuguano mikali hata miongoni mwa watu waliokuwa upande mmoja.
Lissu anapaswa kukalishwa chini akaelezwa shida ya ‘kamdomo’ alikonako. Leo ukimuuliza Mtanzania makini kuwa hivi sera ya Lissu anayoipigania ni ipi? Utapata tabu kupata majibu. Wengi watakwambia anataka CCM iondoke madarakani. Ukiuliza swali la nyongeza kuwa ikiondoka afanye nini? Hakuna mwendelezo.
Mara zote tunaelezwa matusi dhidi ya Rais, anatukana viongozi na watoto wao akiwamo Mbowe, matusi ambayo si sera inayoweza kuliletea maendeleo yoyote taifa letu. Nasema Lissu ukimsikiliza anayo maarifa mengi, ila ametindikiwa busara katika kauli.

Sitanii, najua ukweli huu baadhi ya watu hawataki kuusikia. Wanasiasa wenye kusababisha mipasuko katika jamii mara zote huwa hawafanikiwi kushika madaraka ya juu katika serikali za nchi mbalimbali duniani.
Naamini msomaji unamfahamu mwanasiasa Mfaransa Marine Le Pen. Mama huyu ambaye amepata umaarufu mkubwa nchini Ufaransa kutokana na siasa za ubaguzi, kwamba hataki mtu asiyekuwa Mfaransa kuishi Ufaransa, kwa sasa mahakama ya nchi hiyo imempiga marufuku kushiriki siasa.
Nisikilize tena. Nimesema Lissu anayo akili ila anatindikiwa maarifa. Hii haimaanishi kuwa kila anachokisema hakina maana. Kwa mfano, Lissu na Watanzania wengi wanapinga watu kupotea katika mazingira yasiyoeleweka. Msamiati wa “Watu Wasiojulikana” kwa sasa baada ya kelele umepotea kidogo na kasi ya watu kupotea imepungua kidogo. Si haki kila anayepinga hoja kupotezwa. Hili linajenga chuki kubwa.
Ripoti ya Jaji Chande imesema bayana kuwa taratibu za uchaguzi nchini zimelalamikiwa, kwa muda mrefu zimekuwa chimbuko la chuki inayoendelea kukua. Ni ukweli ulio wazi kuwa kuna majimbo kama Kigoma Mjini, Hai au Pemba, tangu enzi ni majimbo ya upinzani. Leo unakuta anashinda mbunge wa CCM kwa kura ambazo hata aliyeshinda anazishangaa!
Sitanii, siasa si lazima upate kila kitu. Bunge letu lina majimbo 272, kwa maana ya majimbo 222 kwa Tanzania Bara na majimbo 50 kwa Zanzibar. Kama chama tawala kinataka kupitisha uamuzi bungeni kinahitaji theluthi mbili katika masuala magumu. Hivyo kwa lugha rahisi, chama tawala kinahitaji wabunge 181, na kwa uwiano sawa na huo kwa viti maalumu kupitisha ajenda yoyote bungeni.
Najiuliza, kuna sababu gani ya kukomba majimbo yote kwa ufagio? Hivi hatujui kuwa vyama vya siasa ni sehemu ya ajira pana kwa vijana wanaoshinda wanaeneza sera za vyama vyao? Vyama vinapokosa ruzuku vijana hawa wanakuwa hawana cha kufanya zaidi ya kumsaka aliyewakosesha mkate katika familia zao!

Hebu jaribu kuwaza kidogo kwamba leo waajiriwa wote wa CCM itokee CCM ishindwe uchaguzi ofisi zote za kata, wilaya, mikoa na vitengo vyote zifungwe kusiwepo ruzuku, halafu kama imeshinda CHADEMA na mkate wao wana CCM umekoma kuingia kwenye familia zao uwaite na kuwaambia tulinde utulivu na amani! Hali itakuwaje? Geuza shilingi upande wa pili.
Kesi inayomkabili Lissu sipaswi kuijadili kwa mujibu wa Kifungu cha 114(1)(d), kwani ni kesi inayoendelea. Ingekuwa naruhusiwa kuijadili, ningesema kesi hii ingenoga kama Lissu angeshitakiwa kwa uchochezi. Nigesema kesi hii vielelezo vilivyopo itakuwa rahisi ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko Lissu kushindwa kesi hii. Ni bahati mbaya sheria inazuia, na wala sitayasema hayo.
Lakini bado ninayo haki ya kutoa maoni yangu. Kwamba badala ya serikali kuendelea na hii kesi iliyokuwa mzizi wa mpasuko na mwisho wa siku ikatokea, narudia, ikatokea Lissu akawashinda, basi Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) atumie mamlaka aliyonayo kuiondoa hii kesi mahakamani. Hii itakuwa hatua kubwa ya kuponya vidonda. Itakuwa hatua ya kuliunganisha taifa letu, wala isichukuliwe kuwa ni ushindi wa upande wowote, bali kwa taifa letu la Tanzania.
Lakini kama tunataka maridhiano ya kweli, taifa linahitaji kujifunza kusonga mbele bila kubeba chuki za jana. Falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan – maridhiano (Reconciliation), ustahimilivu (Resilience), mageuzi (Reforms) na kujenga upya (Rebuilding) – ilikuwa ishara kwamba Tanzania ilihitaji ukurasa mpya wa siasa.
Hatua ya kuunda kikosi kazi cha kuchunguza hali ya siasa nchini ilikuwa sehemu ya kuonyesha kuwa changamoto za kisiasa zinahitaji majibu ya kitaifa, si ya upande mmoja. Pia haiwezi kupuuzwa hatua ambayo Rais Samia aliyowahi kuchukua baada ya tukio la kupigwa risasi kwa Lissu, alipokwenda kumtembelea hospitalini mara mbili akiwa Nairobi na baadaye Brussels.
Katika mazingira ya kisiasa yenye mvutano mkubwa, hatua hiyo ilikuwa ishara ya kibinadamu, ambayo viongozi wengi hawakuthubutu kuifanya. Ilikuwa ujumbe kwamba tofauti za kisiasa hazipaswi kuondoa utu. Sasa wakati umefika kwa Tanzania kufunga milango ya uhasama wa kisiasa na kufungua milango ya ushindani wa hoja. Taifa haliwezi kujengwa kwa kizazi kinachorithishana hasira za kisiasa.
Tunapaswa kufikia mahali ambapo mtu anaweza kugombea bila kuogopa, kukosoa bila kuhofia, na kushinda bila kuwa na shaka. Uchaguzi unapoitishwa, mshindi anapaswa kutangazwa kwa uwazi na kukubaliwa na wote. Maridhiano si udhaifu. Maridhiano ni ishara ya taifa lililokomaa.
Tanzania haihitaji wanasiasa wanaotafuta kushinda kwa kuangusha nchi; inahitaji viongozi wanaoweza kushindana mchana na kushirikiana pale masilahi ya taifa yanapohitajika. Na hapa nasisitiza, Lissu naamini ananisoma na anakumbuka maneno niliyomwambia kwenye mjadala niliouendesha mwaka jana. Nilimwambia nchi haipati faida yoyote kwa kumwaga damu. Mnaokumbuka mnakumbuka alichonijibu.

Sitanii, Tanzania ni nchi yetu sote. Wakati wa mazungumzo ni sasa. Tusisubiri kila jambo liende mahakamani, kwani kunaweza kutufanya tushinde kesi, lakini tukapoteza taifa. Binafsi naiona nia njema ya Rais Samia. Tangu mwanzo alilenga kuliunganisha taifa. Tusisahau mazingira aliyochukua uongozi Rais Samia. Rais Samia si mwasisi wa msamiati wa “Watu Waisojulikana.”
Tukihesabu watu waliopotea kabla ya Rais Samia kuingia madarakani, tukikumbushana miili iliyokuwa inaokotwa kwenye viroba baharini, kutekwa kwa akina Mo na wengine, mabasi kutotembea usiku kwa hofu ya kutekwa, majambazi kutembeza risasa vituo vya mafuta, benki na baa… panya road walivyokuwa wanasumbua Dar es Salaam, ebu Watanzania tusiwe wasahaulifu.
Sitanii, turekebishe yasiyokubalika, lakini si haki kusema Rais Samia hajatenda kitu. Ikiwa tunafanya kosa la kudhani vyama vinaweza kutumia jinsia kujipatia umaarufu, basi tuvuke huu msitari. Tuanze maridhiano ya kweli sasa kwa kusahihisha aliyosema Jaji Chande. Lissu aachiwe, ila aambiwe achunge ‘kamdomo’. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827

