Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam


Bandari ya Dar es Salaam imeibuka kinara wa ufanisi wa huduma za bandari katika ukanda wa Afrika Mashariki baada ya kupanda kwa nafasi 105 katika Ripoti ya Ufanisi wa Bandari Duniani (Container Port Performance Index – CPPI) ya mwaka 2025, hatua inayodhihirisha mafanikio ya mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya usafirishaji na biashara nchini Tanzania.

Ripoti hiyo, inayotolewa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na S&P Global Market Intelligence, inaonyesha kuwa Bandari ya Dar es Salaam imepanda kutoka nafasi ya 360 mwaka 2024 hadi nafasi ya 255 mwaka 2025 duniani.

Mafanikio hayo yanaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa bandari iliyofanya vizuri zaidi katika Afrika Mashariki kwa mujibu wa viwango vya ufanisi vinavyopima muda wa kuhudumia meli, kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo, pamoja na matumizi bora ya miundombinu ya bandari.

Wakati Dar es Salaam ikionyesha mafanikio hayo, Bandari ya Mombasa, Kenya imepoteza nafasi katika orodha hiyo kwa kushuka kutoka nafasi ya 375 mwaka 2024 hadi nafasi ya 396 mwaka 2025.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamkala ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw Plasduce Mkeli Mbossa amesema kupanda kwa Bandari ya Dar es Salaam ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya bandari kwa miaka ya karibuni ikihusisha miundombinu.

Ametaja uwekezaji huo kuwa ni katika vifaa vya kisasa vya kuhudumia mizigo, pamoja na mageuzi ya kiutendaji yaliyolenga kupunguza muda wa meli kusubiri na kuhudumiwa bandarini.

“Ufanisi wa bandari umeongezeka kwa takribani asilimia 98 kutokana na kupungua kwa muda wa kuhudumia meli.

“Hii ni ishara kwamba Tanzania tumeanza kuvuna matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya bandari chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo kuongezeka kwa ufanisi huu kunamaanisha gharama za usafirishaji zinaweza kupungua, muda wa mizigo kufika sokoni unapungua, na ushindani wa biashara ndani na nje ya nchi unaongezeka,” amesema Bw. Mbossa.

Aidha, Bw Mbossa amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanaweza kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu zaidi la biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hasa wakati mahitaji ya usafirishaji wa mizigo kupitia Bahari ya Hindi yanazidi kuongezeka.

 *Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo Bw. Mbossa ametaja changamoto zilizopo na hatua zinazochukuliwa na TPA.

“Licha ya kupanda, bado tunazo changamoto na tunaelewa mzigo unaongezeka hivyo TPA inachukua hatua kubwa na za makusudi za kupanua miundombinu na katika bandari zake zote ili kuondokana na changamoto zote pamoja na kuhakikisha ukuaji wa uchumi wetu na wa nchi zinazotumia bandari zetu unasaidiwa na bandari bora kabisa,” amesema Bw. Mbossa.*

Matokeo ya CPPI 2025 yanaweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuimarisha hadhi yake kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki, huku Bandari ya Dar es Salaam ikionekana kuwa miongoni mwa bandari zinazokua kwa kasi zaidi katika bara la Afrika.

Kwa wataalamu wa uchumi wa bahari na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki, matokeo haya yanaashiria mabadiliko makubwa ya ushindani wa bandari za eneo hili. 

Kwa miaka mingi, Dar es Salaam na Mombasa zimekuwa zikishindana kuvutia shehena za nchi zisizo na bandari kama Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Rwanda, Uganda na Malawi.