Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kongwa
Rais wa Namibia, Dk. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema Tanzania na Namibia zina wajibu wa kuendeleza na kuimarisha uhusiano wao wa kihistoria uliojengwa wakati wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika, ili uwe chachu ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.
Dkt. Nandi-Ndaitwah alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Dodoma, ambapo alitembelea Kambi ya Wapigania Uhuru wa Namibia iliyopo Kongwa pamoja na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Namibia katika Mji wa Serikali Mtumba.
Akiwa Kongwa, Rais huyo aliweka mashada ya maua katika makaburi ya mashujaa wa Namibia waliopoteza maisha wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi yao, huku akipata fursa ya kutembelea makazi na hospitali iliyokuwa ikitoa huduma za matibabu kwa wapigania uhuru hao walipokuwa wakihifadhiwa nchini Tanzania.
Pia alikutana na familia zenye asili ya Namibia zinazoishi Kongwa na kuzungumza na wananchi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla iliyofanyika katika eneo la makaburi ya mashujaa hao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Nandi-Ndaitwah aliishukuru Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika ukombozi wa Namibia, akieleza kuwa Kongwa ni sehemu yenye historia muhimu katika safari ya taifa hilo kuelekea uhuru.
Alisema eneo hilo lina nafasi ya pekee katika mioyo ya wananchi wa Namibia kutokana na mchango wake katika kuwapa mafunzo na hifadhi wapigania uhuru wa nchi hiyo.
“Tunathamini mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Namibia. Kongwa ni sehemu ya historia yetu na kwa wananchi wa Namibia eneo hili ni kama nyumbani kwao,” alisema.
Rais huyo alisisitiza kuwa historia ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili inapaswa kuhifadhiwa na kuenziwa, huku akitoa wito wa kuendelezwa kwa ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Alibainisha kuwa Tanzania na Namibia zina fursa kubwa za kushirikiana katika nyanja za biashara, uwekezaji na maendeleo ya kijamii ili kuongeza ustawi wa wananchi wa nchi hizo mbili.
Ziara ya Rais Nandi-Ndaitwah imeonekana kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Namibia, huku ikikumbusha mchango wa mataifa hayo katika harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.










