Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, ameitaka jamii na wadau
mbalimbali kushirikiana na Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) katika
mapambano dhidi ya bidhaa bandia ili kulinda afya za wananchi na
uchumi wa taifa.
Mapunda alitoa wito huo wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya
Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani yaliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt
Regency jijini Dar es Salaam na kuandaliwa na FCC.
Amrsema kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia yanahitaji nguvu ya
pamoja kwa kuwa wahusika wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa hizo
wanapatikana katika maeneo mbalimbali nchini.
“FCC peke yake haiwezi kumaliza tatizo hili,tunahitaji ushirikiano wa
wananchi, wafanyabiashara, sekta binafsi na taasisi nyingine ili kudhibiti bidhaa bandia zisiweze kuingia katika soko na kuhatarisha maisha ya watu,”amesema.
Aidha, aliitaka FCC kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya
bidhaa bandia kupitia kampeni za kitaifa, pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa hizo hususan katika masoko na mipaka ya nchi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa,
amesema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuimarisha ushirikiano kati
ya wadau mbalimbali katika kupambana na bidhaa bandia.
Amesema suala la bidhaa bandia linahitaji ushiriki wa jamii nzima
kutokana na athari zake kwa afya ya wananchi na uchumi wa nchi.
Ngasongwa amesema FCC imeendelea kupata mafanikio katika operesheni
zake, ikiwemo kukamata viwanda haramu vya kutengeneza pombe pamoja na shehena za sigara na vilainishi bandia.
“Lengo letu ni kuhakikisha walaji wanapata bidhaa salama na zenye
viwango stahiki,kwani bidhaa bandia zinaweza kusababisha madhara
makubwa kwa afya na usalama wa watumiaji,” amesema.
Amedai kuwa FCC imeimarisha udhibiti katika bandari na bandari kavu
kwa kuweka wakaguzi maalumu na kutumia mifumo ya kidijitali kufuatilia
bidhaa zinazoingia nchini kabla hazijaingia sokoni.
Pia amewataka wamiliki wa alama za biashara kuzisajili katika FCC ili
kurahisisha utambuzi wa bidhaa halisi na bandia wakati wa ukaguzi.
Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Jaji Rose Ebrahim, amesema FCC imeandaa mpango mkakati mpya unaolenga kuongeza uwezo wa kugundua, kuzuia na kuondoa bidhaa bandia sokoni kwa wakati.
Amesema mpango huo pia unalenga kuimarisha ushirikiano na wamiliki wa
alama za biashara, kuongeza elimu kwa umma na kutumia teknolojia za
kisasa katika shughuli za ukaguzi na uchunguzi.
Kwa mujibu wa Jaji Ebrahim, mpango huo umezingatia changamoto
zilizojitokeza katika miaka ya hivi karibuni, ikiwemo ukuaji wa
biashara za kidijitali, mbinu mpya za usambazaji wa bidhaa bandia na
uhitaji wa teknolojia za kisasa za uchunguzi.
Amesema FCC itaendelea kuimarisha uratibu na taasisi nyingine za
udhibiti, kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia
na kuongeza matumizi ya TEHAMA ili kudhibiti kwa ufanisi biashara ya
bidhaa bandia nchini.







