📌Afungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, Dodoma

📌Asisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa mapato

📌Awapongeza kwa kazi nzuri na kuendelea kuimarisha mahusiano na wadau

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, ametoa rai kwa mameneja wa TANESCO nchini kusimamia na kupambana kwa nguvu zote na changamoto ya wizi wa miundombinu ya umeme, ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali ya mikoa wanayoisimamia.

Bw. Twange ameyasema hayo Juni 24, 2026, mkoani Dodoma wakati akifungua Mkutano mkuu wa mwaka wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, wenye lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Shirika pamoja na Kurugenzi ya Usambazaji.

Licha ya kuwapongeza mameneja hao kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwahudumia wananchi, amesema kuna haja ya kila mmoja kuona uchungu wa mali za Shirika kwa kuongeza jitihada za kuhakikisha changamoto ya wizi wa miundombinu ya umeme inatokomezwa.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya. Mara nyingi tunapongezwa kwa utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Sasa ongezeni kasi ya kuhakikisha mali za Shirika zinalindwa. Pambaneni na changamoto ya wizi wa vifaa vya umeme, kwani matukio kama haya hayaleti taswira nzuri kwa Shirika,” alisisitiza Bw. Twange.

Katika Mkutano huo , Bw. Twange pia ameeleza umuhimu wa kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa shughuli nyingi zinazofanywa na Shirika katika kuwahudumia wananchi hutegemea mapato yanayokusanywa.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Manyara, Mha. Regina MVungi amesema Mkutano huo unekuwa na mchango mkubwa katika kutathmini utendaji kazi pamoja na utekelezaji wa mpango mkakati wa Shirika. Huku Meneja wa TANESCO Ruvuma Mha. Eliseus Mhelela ameeleza namna walivyojipanga kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji ili kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.

Mkutano huo wa Mameneja na Wakurugenzi wa Kanda, umewashirikisha pia Mameneja Wakuu wa Kampuni Tanzu za TANESCO, umeanza rasmi Juni 24, 2026, na unatarajiwa kuhitimishwa Juni 26, 2026.