Mbunge wa Jimbo la Ismani, Mheshimiwa Emmanuela Mtatifikolo, ameendelea kutekeleza ahadi yake ya kuwagusa wananchi wa kila eneo kwa kugawa viti mwendo kwa watu wenye mahitaji maalum, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha maisha yao na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao za kila siku bila changamoto.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Mtatifikolo amesema ameanza na eneo la Kitanewa, Kata ya Idodi, ambapo wananchi wenye uhitaji wamekabidhiwa viti mwendo vitakavyowarahisishia kufanya shughuli zao kwa uhuru na ufanisi zaidi.

Ameeleza kuwa mpango huo utaendelea kufikia maeneo mengine ya Jimbo la Ismani, huku akisisitiza dhamira yake ya kuwafikia makundi mbalimbali yenye mahitaji maalum ili kuendelea kuleta faraja na kuboresha ustawi wa wananchi.

Aidha, amewaomba wananchi wa Jimbo la Ismani kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa bidii na kudumisha mshikamano ili kuharakisha maendeleo ya jimbo hilo.

Akihitimisha, Mheshimiwa Mtatifikolo amesisitiza kuwa ataendelea kuwa sauti ya wananchi wa Ismani na kutetea maslahi yao, akitekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuwaongoza.