Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya ya Butiama Kizurira Nyerere wilayani Butiama, mkoani Mara, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hospitali hiyo imejengwa kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Wilaya ya Butiama na maeneo ya jirani, ambapo awali walilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika hospitali za wilaya nyingine.
Taarifa ya mradi iliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, Dkt. Sunday Mwakyusa, pamoja na maelezo ya kiufundi yaliyotolewa na Mhandisi Peter Maga, ilieleza kuwa hadi sasa Halmashauri imepokea jumla ya shilingi bilioni 3.66 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, fedha zilizotolewa na Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri. Ujenzi unaendelea kwa mfumo wa Force Account, huku baadhi ya majengo yakikamilika na kuanza kutoa huduma na mengine yakiwa katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Majengo yaliyokamilika ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, jengo la dharura, jengo la upasuaji, wodi ya wazazi na kichomea taka za hospitali. Aidha, ujenzi wa jengo la utawala, wodi za wanaume na wanawake, jengo la mionzi, bohari ya dawa na kufulia unaendelea.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya afya nchini.
Alisema hadi mwaka 2020 kulikuwa na hospitali za halmashauri 55 pekee tangu Uhuru, lakini katika kipindi cha miaka sita ya Serikali ya Awamu ya Sita zimejengwa hospitali za halmashauri 129, hatua iliyowezesha halmashauri zote 184 nchini kuwa na hospitali zenye miundombinu bora na ya kisasa.
Aidha, alisema Serikali imetenga shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kukamilisha majengo yaliyosalia katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama ili huduma zote muhimu zianze kutolewa kwa wananchi.
Hospitali hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za wagonjwa wa nje, upasuaji, huduma za mama na mtoto, maabara, mionzi, tiba ya viungo pamoja na huduma nyingine muhimu za kibingwa, hivyo kupunguza rufaa zisizo za lazima kwenda hospitali za nje ya wilaya.



