Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema mchakato unaoendelea wa maridhiano ya kisiasa unatarajiwa kuimarisha umoja wa kitaifa, kurejesha imani ya wananchi na kuweka mazingira bora zaidi kwa ukuaji wa uchumi, uwekezaji na maendeleo ya kijamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa Azimio la Pamoja leo Julai 9, 2026 katika viwanja Ikulu Zanzibar, lililoashiria kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mchakato wa maridhiano, Dk. Mwinyi amesema hatua hiyo ni mafanikio muhimu katika utekelezaji wa masharti ya Katiba yanayohusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).
“Utaratibu huu unaakisi dhamira ya serikali yangu ya kuimarisha umoja, maridhiano na ushirikiano miongoni mwa Wazanzibari kwa manufaa ya wananchi wote,” amesema.
Rais Mwinyi pia aliahidi kushirikiana kwa karibu na viongozi wa vyama vya siasa katika kusimamia awamu ya pili ya mchakato huo, ambayo itahusisha majadiliano kuhusu ajenda zilizokubaliwa.
Ameeleza imani yake kuwa pande zote zitaweka mbele maslahi ya Zanzibar na kufikia mwafaka wa kudumu.
Amesema maridhiano yatakapofanikiwa yataongeza imani ya wananchi, wawekezaji, wafanyabiashara na washirika wa maendeleo, hivyo kuendelea kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Zanzibar katika mazingira ya amani na utulivu.
Aidha, Rais Mwinyi ameataka viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuunga mkono mchakato huo, akisisitiza kuwa maendeleo endelevu yanaweza kupatikana tu pale ambapo kuna amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Pia alikumbusha kuwa Zanzibar imewahi kuonyesha kuwa maridhiano ya kisiasa yanaweza kufanikiwa, akitolea mfano maridhiano ya mwaka 2001 yaliyoweka msingi wa marekebisho ya Katiba na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Ameongeza kuwa uzoefu wa marais wastaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein, unaendelea kutoa mwongozo muhimu katika kuendeleza mchakato wa sasa wa maridhiano.




