Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo wamezindua rasmi hatua mpya ya maridhiano ya kisiasa yenye lengo la kuimarisha amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kudumu Zanzibar.

Hatua hiyo imeashiriwa na kutiwa saini kwa tamko la pamoja kati ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa niaba ya CCM Zanzibar, na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Othman Masoud Othman.

Akilisoma tamko hilo leo Julai 9, 2026, katika viwanja Ikulu Zanzibar, Katibu wa Kamati ya Maridhiano, Mansura Mosi Kassim, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya mazungumzo ya kina yaliyofanyika chini ya mwongozo wa marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk. Ali Mohamed Shein.

Amesema tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, chaguzi mbalimbali zilizofanyika Zanzibar zimekuwa zikikumbwa na mvutano wa kisiasa uliosababisha migawanyiko na kuathiri juhudi za maendeleo.

Mansura amesema ingawa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ulifanyika katika mazingira ya amani, baadhi ya vyama vya siasa vilibaki na hoja zilizoathiri mchakato wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Amewleza kuwa kufuatia ushauri wa marais wastaafu, CCM na ACT Wazalendo zilianza mazungumzo ya kutafuta suluhisho la kudumu.

Mazungumzo hayo yalijumuisha mikutano tisa iliyofanyika kati ya Novemba 2025 na Aprili 2026, ambayo ilisaidia kupunguza tofauti zilizokuwepo kati ya pande hizo mbili.

Kwa mujibu wa tamko hilo la pamoja, vyama hivyo viwili vimekubaliana kuunda Kamati ya Pamoja ya Majadiliano itakayosimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa, huku mchakato huo ukitarajiwa kuwashirikisha wananchi, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wengine.

“Maridhiano haya yanalenga kujenga mwafaka wa kweli wa kitaifa, kuimarisha demokrasia, utawala bora na kuheshimu utawala wa sheria,” lilisema tamko hilo.

Tamko hilo pia lilieleza kuwa mfumo maalumu wa kisheria utaanzishwa ili kuratibu na kusimamia utekelezaji wa makubaliano yote yaliyofikiwa, huku viongozi wakisisitiza kuwa maslahi ya Zanzibar yataendelea kutangulizwa mbele ya maslahi ya chama chochote cha siasa au mtu binafsi.

CCM na ACT Wazalendo kwa pamoja wamewaomba Wazanzibari kuunga mkono mpango huo wa maridhiano, wakisema umoja, amani na utulivu ni msingi muhimu wa kuharakisha maendeleo na kujenga mustakabali bora wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.