Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kali kwa watu na makundi yanayojihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua madhubuti kulinda raia, maisha yao na mali zao.

Akizungumza Zanzibar wakati wa utiaji saini wa tamko la pamoja leo Julai 9, 2026 katila viwanja vya Ikulu Zanzibar kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo, Rais Samia amesema Tanzania haitavumilia vitendo vinavyojificha chini ya mwamvuli wa uanaharakati ilhali lengo lake ni kusababisha vurugu, kuharibu mali au kuvuruga utulivu wa taifa.

Rais ameaema baadhi ya watu hujiwasilisha kama wanaharakati, lakini matendo yao ni ukiukwaji mkubwa wa amani na usalama, ikiwemo uharibifu wa miundombinu, kuvuruga utaratibu wa umma na kujaribu kuishinikiza Serikali kwa njia zisizo halali.

“Mtu anayeipenda kweli nchi yake huijenga, haibomoi,” amesema Rais Samia.

Aidha, aliwataka wananchi kukataa vitendo vinavyodhoofisha utulivu wa taifa na maendeleo yake.

Amesema Watanzania wanahitaji amani, usalama na mazingira yanayowawezesha kufanya shughuli za kiuchumi, kupata huduma muhimu na kuboresha maisha yao, badala ya vurugu na migogoro ya kisiasa isiyoisha.

Rais aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kulinda usalama wao na mali zao, akisisitiza kuwa jukumu la kudumisha amani linapaswa kutekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi.

“Serikali iko imara katika kulinda wananchi wake na mali zao. Nanyi wananchi shirikianeni na Serikali kulinda jamii zenu na rasilimali za taifa,” amesema.

Akiwaonya wanaojaribu kuchochea migogoro na machafuko nchini, Rais Samia alisema hakuna taifa linaloruhusu shughuli zinazohatarisha maisha ya watu wake na usalama wa nchi, akiongeza kuwa Tanzania itatumia hatua za kisheria kulinda amani na heshima ya taifa.

Amesisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanategemea mazingira ya amani na kwamba tofauti za kisiasa zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na maridhiano badala ya vitendo vinavyodhuru jamii.

“Amani ndiyo mtaji wetu, maridhiano ndiyo daraja letu, na wananchi ndiyo sababu ya uongozi wetu,” amesema Rais Samia.