Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed, amesema Zanzibar ina nafasi kubwa ya kuimarisha uchumi wake kupitia biashara, utalii na utamaduni, huku akisisitiza umuhimu wa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Zanzibar yaliyofanyika ndani ya Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Ayoub alisema licha ya ukubwa mdogo wa kijiografia wa Zanzibar, visiwa hivyo vina historia na uwezo mkubwa wa kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji.
“Tukubali kwamba kwa ukubwa wa eneo, Zanzibar ni ndogo, lakini kwa ubora wa bidhaa na huduma, Zanzibar ni kubwa zaidi ya tunavyofikiria. Twende tukashindane kwa ubora wa bidhaa, ubora wa vifungashio na ubora wa utoaji wa huduma,” alisema Ayoub.
Alisema historia ya Zanzibar kama lango la biashara katika Bahari ya Hindi inapaswa kuendelea kutumika kuvutia wawekezaji na kufungua masoko mapya ya bidhaa na huduma zinazozalishwa visiwani.
Aidha, alisema maadhimisho ya miaka 50 ya Maonyesho ya Sabasaba yameendelea kuthibitisha mchango wake katika kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi, huku Zanzibar ikiendelea kunufaika kwa kutangaza bidhaa zake pamoja na ubunifu wa wananchi wake.
“Maonyesho haya ni jukwaa muhimu la kutangaza fursa zilizopo Zanzibar na kuwakutanisha wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema.
Ayoub alieleza kuwa utamaduni wa Zanzibar ni rasilimali muhimu ya kiuchumi inayoweza kuongeza mapato kupitia sekta za utalii, sanaa na biashara. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mavazi ya asili, muziki wa taarabu na mila mbalimbali kama sehemu ya vivutio vya utalii.
Vilevile, alihimiza kuendelea kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kama nyenzo muhimu ya biashara na utalii, akisema imeendelea kufungua fursa za ajira na kukuza uchumi ndani na nje ya Tanzania.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake, akisema umeendelea kuhakikisha nchi inabaki salama na yenye mazingira rafiki kwa biashara na uwekezaji.
“Amani na utulivu ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi. Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira yanaendelea kuwa salama ili wafanyabiashara na wawekezaji wafanye shughuli zao kwa uhakika,” alisema.
Hata hivyo aliwataka wawekezaji na wafanyabiashara kutumia kikamilifu fursa zilizopo Zanzibar ili kujenga ushirikiano utakaokuza biashara, uwekezaji na uchumi endelevu kwa manufaa ya wananchi.




