Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kilombero
WAZIRI wa Ujenzi, Abdalah Ulega amempongeza Mbunge wa Mlimba (CCM), Dk Kellen- Rose Rwakatare kwa namna ambavyo amekuwa akiwasilisha kero za wananchi wa jimbo hilo kwenye mamlaka ili zipate ufumbuzi.
Alitoa pongezi hizo jana wakati wa ziara yake ya kukagua barabara za Wilaya ya Kilombero ambapo alifika kwenye jimbo la Mlimba na kuzungumza na wananchi wa jimbo hilo pamoja na Mbunge huyo.
“Kwa namna ya kipekee mimi nanyinyi tumshukuru Mbunge wenu, Dk Kellen Rose Rwakatare maana amekuwa mtumishi mwema wa kupeleka habari za maendeleo, nyingi watu wa Mlimba mna mtu mzuri wa kufanya kazi hiyo, meseji zake ni nyingi sana hapa kwangu za kutaka barabara,” alisema
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mbunge huyo alisema mkandarasi anayetengeneza barabara yao ya kipande cha Ifakara Mbingu amekuwa akisua sua kwa muda mrefu.
“Mheshimiwa Waziri leo uko hapa na mkandarasi yuko hapa tunaomba ama atengeneze barabara yetu au arejeshe fedha zetu tumechoka kuona barabara haipitiki na mkandarasi hafanyi lolote,” alisema
“Kama anasema atajenga basi asimame hapa mbele yako mheshimiwa Waziri aseme kwa dhati kabisa ataanza kuijenga lini hii barabara maana imekuwa kero kwa wananchi wangu wa Mlimba,” alisema Dk Rwakatare.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa nawewe uko hapa naona hawa watu wanatuchezea sana wakiendelea hivi tunakuomba sweka ndani, mimi nikakaangwa kila siku na wananchi wangu wa Mlimba, kila kukicha ni maneno yah ii barabara kwa hiyo naomba atuambie ataijenga lini,” alisema Dk Rwakatare












