Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora limekamata watuhumiwa watatu kwa tuhuma za kupanga njama ya kufanya utapeli katika benki za CRDB na NMB zilizoko Mjini Tabora.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa ACP Twaha Lulengelule amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao Julai 10 mwaka huu majira ya saa 3:50 asubuhi walipokuwa wakijiandaa kuvamia benki hizo.
Ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa na askari waliokuwa doria katika maeneo ya benki wakati wakijiandaa kutekeleza azma yao ya kuingia na kupora wateja waliokuwa ndani ya benki hizo.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Shabani Nyambi (36), mkazi wa Kimara Korogwe, Dar es salaam, Saidatu Masoud (52) na Veronica Richard (40), wakazi wa Kimara Temboni, Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Kamanda amefafanua kuwa baada ya kupekuliwa walikutwa na dola 7 za kimarekani, madaftari madogo 6, bahasha za kaki 8 pamoja na karatasi zilizokatwa kwa ukubwa unaolingana na noti za dola ambazo hutumika kuhadaa wateja.
‘Baada ya kukamatwa watuhumiwa hao walikiri kuhusika na matukio ya utapeli ikiwemo kupanga njama za kuingia ndani ya benki kwa lengo la kutapeli wateja ili kujipatia fedha isivyo halali’, ameongeza Kamanda.
Watuhumiwa hao pia wamekuwa wakitumia mbinu ya kumfuatilia mteja anayetoa fedha nyingi benki na kumshawishi wambadilishie kwa fedha za kigeni kwa bei nafuu ambapo humpatia noti bandia za dola na kisha kutoroka.
Kamanda ametoa wito kwa jamii kuwa makini na watu wasiowafahamu wanaowafuata baada ya kutoa fedha benki na kuwashawishi kufanya biashara au kubadilishana fedha nje ya utaratibu rasmi wa taasisi za kifedha.



