NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Utafiti uliofanywa katika wilaya tatu nchini umebaini kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri miundombinu ya shule, huku maeneo yanayokumbwa na mafuriko yakitajwa kuwa katika hatari kubwa ya kuharibika kwa madarasa, maktaba, maabara na miundombinu mingine ya shule.
Akizungumza kuhusu utafiti huo, mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Simon Ngalomba, amesema utafiti huo ulilenga kuchunguza athari za mabadiliko ya tabianchi katika shule pamoja na kiwango cha utayari wa shule na jamii zinazozunguka kukabiliana na athari hizo.
Amesema baadhi ya shule zimeanza kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo upandaji wa miti katika maeneo ya shule ili kupunguza athari za upepo mkali na kuboresha mazingira.
Hata hivyo, amesema bado kuna uhitaji wa kuongeza elimu kwa wanafunzi, walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kuhusu namna bora ya kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Boniface Tobias kutoka Tanzania Youth and Children (TYC), amesema utafiti huo umetoa mwanga kwa mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.
Amesema taarifa zilizopatikana kupitia utafiti huo zitasaidia wadau kushirikiana na Serikali katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili watoto shuleni, hususan zile zinazochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.
Utafiti huo pia umeangazia ushirikishwaji wa makundi maalum katika mipango na maamuzi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti, makundi hayo, hususan watu wenye mahitaji maalum, bado hayashirikishwi kwa kiwango cha kutosha katika mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Shirika la Macho kwa Jamii Theresia Lihanjala, amesema makundi maalum yanapaswa kushirikishwa kuanzia hatua za kubuni mipango, kupanga hadi kufanya maamuzi, kwa kuwa wao ndio wanaofahamu kwa kina changamoto wanazokutana nazo.
Amesema kutoshirikishwa kwa makundi hayo kunaweza kusababisha mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kutokidhi mahitaji halisi ya watu wote.
Ametoa mfano kuwa mtu mwenye ulemavu wa kutembea anaweza kukumbana na changamoto tofauti wakati wa mafuriko au majanga mengine ikilinganishwa na mtu asiye na ulemavu, hivyo uzoefu wao ni muhimu katika kubuni mikakati itakayohakikisha usalama wa kila mmoja.
Wadau hao wamezitaka Serikali na taasisi zinazohusika kuhakikisha elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi inaendelea kutolewa katika shule na jamii, huku makundi maalum yakipewa nafasi kubwa zaidi katika kupanga na kutekeleza mikakati ya kukabiliana na athari hizo.



