Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeshauri kuwa miradi ya biashara ya kaboni iendelee kuwanufaisha wananchi hususani mwananchi mmoja mmoja katika maeneo yanayotekeleza miradi hiyo.
Kamati hiyo imebainisha kuwa ni vyema maeneo yanayotekeleza miradi ya Biashara ya Kaboni ikiwemo miradi ya misitu yakasimamiwa vyema hususan mikataba inayosimamia miradi ya kaboni iweze kuwanufaisha wananchi wanaozungukaa maeneo hayo.
Hayo yamebainika wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake ambayo iliwasilishwa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo Agosti 13, 2026.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga aliipongeza NCMC kwa kuendelea kuzijengea uwezo jamii zinazotekeleza f pembeni ya misitu kwa kuieletea miradi ya kuiwezesha kutunza misitu misitu.
Alisema kupitia Kituo hicho inapaswa kuwe na utaratibu mahsusi wa kuhakikisha kuwa mavuno au faida zinazopatikana kupitia biashara hiyo zinakuwa endelevu kwa kuwa kila mwaka misitu inazidi kustawi.
“Tuhakikishe kuwa biashara hii inakuwa ya uwazi huku tukifuatilia mikataba inayosainiwa iwe yenye kuwanufaisha wananchi moja kwa moja hasa wale wanaoishi kando ya misitu ambao ndio wanaoitunza,” alisema Mhe. Kiswaga ambaye pia ni mbunge wa Kalenga.
Akitoa ufafanuzi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa alisema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha uratibu na usimamizi wa miradi ya biashara ya kaboni.
Alifafanua kuwa katika katika bajeti ya mwaka 2026/27 tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetenga zaidi ya shilingi bilioni 5 ili zisaidie kujenga mfumo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchukuaji wa takwimu za mtiririko wa uendeshaji wa biashara ya kaboni.
Mhe. Kwagilwa aliongeza kuwa katika kuhakikisha uratibu wa biashara ya kaboni unakuwa endelevu, unawafikia wananchi na kuwanufaisha Serikali inahakikisha inaboresha sekta ya rasilimaliwatu katika eneo hilo.
Kwa upande wake Mbunge wa Lupa Mhe. Masache Kasaka alishauri Ofisi ya Makamu wa Rais kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa na mitaala ya shule mahsusi kwa ya kuwajengea uelewa wanafunzi kuhusu utunzaji wa misitu.
Sanjari na hilo, alihimiza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia katika maeneo hususan ya vijiji uwe wa uhakika na wa gharama ambayo wananchi wanaweza kuimudu kuwa hivyo kuwawezesha waachane na matumizi ya nishati chafuzi wa mazingira.
Itakumbukwa kuwa, Tanzania inatumia biashara ya kaboni kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiongozwa na NCMC chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa mujibu wa Kanuni za 2022 na marekebisho ya 2023.






