Na. Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Benki ya Dunia imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kuendeleza miradi ya kimkakati inayolenga kutumia fursa zilizopo katika Ushoroba wa Kati (Central Corridor) ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania na nchi jirani.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake nchini Tanzania.
Dkt. Diop alisema Benki ya Dunia imeona umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika kuendeleza Ushoroba wa Kati na kuugeuza kutoka kuwa njia ya usafirishaji na kuwa ushoroba wa kiuchumi wenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na kuchochea shughuli za uzalishaji ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maaendeleo ya Taifa 2050.
Alisema kuwa ushirikiano huo utajikita katika kuwekeza na kusaidia maendeleo ya miundombinu muhimu, ikiwemo bandari na reli, pamoja na kupanua mtandao wa reli kuelekea nchi jirani ya Burundi.
“Moja ya maeneo makubwa ya ushirikiano wetu katika siku zijazo ni kuimarisha miradi katika Ushoroba wa Kati, ambapo tumekuwa na majadiliano mazuri na Mhe. Waziri wa Fedha, kuhusu kile tunachoweza kufanya kwa pamoja kuunga mkono ushoroba huu na kuugeuza kuwa wa kiuchumi utakaoweza kutengeneza ajira nyingi,” alisema Dkt. Diop.
Alisema kuwa mbali na miundombinu ya usafirishaji, Benki ya Dunia inaona umuhimu wa kuwa na uwekezaji shirikishi katika maeneo mbalimbali yanayopitiwa na Ushoroba wa Kati, ili kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa nchini ambazo ni pamoja na kilimo, uchakataji wa mazao, uchimbaji na uchakataji wa madini, ujenzi wa vituo vya huduma za usafirishaji na ugavi (logistics hubs), na kuwezesha wananchi kunufaika zaidi na uwekezaji huo.
Aidha, alisema uwekezaji wa aina hiyo ukishirikisha pia sekta binafsi, utasaidia Tanzania na nchi jirani kuongeza thamani ya bidhaa badala ya kusafirisha malighafi pekee, hatua itayochochea uzalishaji, biashara na ajira.
“Ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Tanzania utaendelea kuongozwa na dhamira ya pamoja ya kuwekeza katika maeneo yatakayosaidia kuunda ajira nyingi na zenye tija, hasa wakati Tanzania ikiendelea kukabiliana na mabadiliko ya ongezeko la idadi ya watu” alisema Dkt. Diop.
Akifafanua kuhusu mkakati wa ushirikiano, Dkt. Diop alisema Benki ya Dunia imepata ridhaa ya Bodi yake kuendelea kutumia Mkakati wa Ushirikiano wa Nchi (Country Partnership Strategy) kama mfumo mkuu wa kuongoza ushirikiano wake na Tanzania, huku kukiwa na maboresho katika maeneo ya kipaumbele, ambapo maboresho hayo yataongeza msisitizo katika maendeleo yanayomlenga mwananchi, hususan elimu, afya na ulinzi wa kijamii, pamoja na kukuza sekta binafsi, jambo litakalohitaji uwekezaji zaidi katika nishati na usafirishaji.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amesema kuwa kipaumbele cha Tanzania ni kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Benki ya Dunia katika kukuza uchumi.
Mhe. Balozi Omar, alisema kuwa Serikali itaendelea kutengeneza mazingira ya kuendeleza sekta binafsi na kuimarisha ushirikiano na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), pamoja na Benki ya Dunia ikiwemo kufanya mageuzi ya ndani yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Ushirikiano huu ni muhimu katika kutekeleza vipaumbele vya maendeleo vya Tanzania, hasa miundombinu, ikiwemo nishati, barabara na bandari, na nawashukuru Benki ya Dunia pamoja na washirika wengine wa maendeleo kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kutekeleza miradi na mageuzi mbalimbali yanayolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi” alisema Mhe. Balozi Omar.
Uwekezaji wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Kupitia Dirisha la IDA umefikia dola za Marekani bilioni 8.96 ukihusisha miradi 35 ambapo miradi 32 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani 8.78 ni ya kitaifa na miradi mitatu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 0.18 ni ya kikanda.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Katibu Mkuu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini, Bw. Firas Raad, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uchambuzi wa Sera, Bw. Juma Mkabakuli na maafisa wengine waandamizi wa Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia kutoka Washington D.C.










