Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

WATU wawili ambao ni askari wa Jeshi la Polisi wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari katika kivuko cha waenda kwa miguu eneo la Maili Moja, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 25, 2026 majira ya saa 1:40 usiku katika barabara kuu ya Dar es Salaam–Morogoro, baada ya gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T.804 ERM kuwagonga askari hao waliokuwa wakivuka katika kivuko hicho.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Josia Isaya Arute, mwenye umri wa miaka 34, mkazi wa Mlandizi, likitokea Dar es Salaam kuelekea Mlandizi.

Inadaiwa dereva huyo alipofika katika eneo hilo, alilipita kundi la magari yaliyokuwa yamesimama kupisha waenda kwa miguu kuvuka, kabla ya kuwagonga askari hao.

Katika ajali hiyo, askari Izdory George Michael alifariki dunia papo hapo, huku askari wa kike, Rehema Juma Magawa, akijeruhiwa kichwani na kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tumbi kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia asubuhi ya Agosti 26 akiwa hospitalini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tumbi, ikisubiri taratibu za kusafirishwa kwenda makwao kwa ajili ya mazishi.

Morcase amesema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi lilifanya msako wa gari hilo baada ya dereva kukimbia eneo la ajali, na kwamba lilikamatwa majira ya saa 2:40 usiku katika eneo la Kwa Mfipa, Wilaya ya Kibaha, likiwa limefichwa, kabla ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi Kibaha kwa ajili ya hatua za kisheria.

Kamanda Morcase amewaonya madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litachukua hatua kali za kisheria dhidi ya madereva wazembe na wanaopuuza michoro na alama za barabarani ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.