Dar es Salaam, Tanzania | 08 Septemba 2026 – Asasi za kiraia na wadau mbalimbali wanakutana kwa ajili ya Jukwaa la Ushirikishwaji wa Asasi za Kiraia Tanzania kuhusu Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS), lenye kaulimbiu “Kuimarisha Hatua Zilizoratibiwa za Asasi za Kiraia katika Kusaidia Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Tanzania wa Wanawake, Amani na Usalama.”

Jukwaa hili limeitishwa kwa pamoja na UN Women na Global Peace Foundation (GPF) Tanzania, kwa msaada wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, na linawakutanisha washiriki takribani 60 kutoka asasi za kiraia, mashirika ya haki za wanawake, asasi za kijamii za ngazi ya jamii na zinazoongozwa na vijana, serikali, taasisi za kitaaluma, mashirika ya kidini, vyombo vya habari, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wa maendeleo.

Jukwaa hili linafanyika katika kipindi muhimu kufuatia kupitishwa kwa Mpango wa Taifa wa Tanzania wa Wanawake, Amani na Usalama (TNAP-WPS) 2025-2029, unaotoa mwongozo wa kitaifa wa kuendeleza amani endelevu, usawa wa kijinsia, utawala shirikishi na ushiriki wenye maana wa wanawake katika michakato ya amani na usalama.

Nchini Tanzania, asasi za kiraia tayari zinatoa mchango muhimu katika ujenzi wa amani, uongozi wa wanawake, ushiriki wa vijana na kuimarisha mshikamano wa kijamii. Jukwaa hili linakusudia kuunganisha juhudi hizo kwa kuweka nafasi ya mashirika kushirikishana uzoefu, kubainisha vipaumbele vya pamoja na kutafuta namna bora ya kushirikiana katika kuendeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama nchini Tanzania.

Moja ya matokeo muhimu yanayotarajiwa kutoka katika Jukwaa hili ni kujenga mwafaka kuelekea kuanzishwa kwa Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Tanzania wa 1325 (Tanzania 1325 CSO Network) – utaratibu wa kitaifa unaomilikiwa na wadau wa ndani utakaowezesha asasi za kiraia kushirikiana, kubadilishana maarifa, kusaidia utekelezaji na ufuatiliaji wa TNAP-WPS, pamoja na kushiriki kwa pamoja katika mijadala ya sera na uwajibikaji.

Ushiriki huo pia utahusisha kutambua na kuweka pamoja mchango uliopo wa asasi za kiraia katika Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, kuandaa mapendekezo ya kuimarisha uratibu, na kuandaa rasimu ya mpango wa hatua (roadmap) kuelekea kuanzishwa kwa Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Tanzania wa 1325.

Baada ya Jukwaa hilo, UN Women na GPF Tanzania zitaendelea kusaidia utekelezaji wa hatua zitakazokubaliwa, ikiwemo mashauriano kuhusu muundo wa uongozi na uanachama wa Mtandao huo, uandaaji wa Masharti ya Kazi (Terms of Reference) na mpango kazi, pamoja na kuweka utaratibu wa muda wa uratibu wakati wa hatua za awali za uanzishwaji wa Mtandao.

Jukwaa hili ni hatua muhimu kuelekea kujenga harakati imara, iliyoratibiwa na inayomilikiwa kitaifa ya asasi za kiraia, yenye uwezo wa kuendeleza kwa pamoja Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama na kuchangia katika kujenga amani endelevu na maendeleo shirikishi nchini Tanzania.