Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
JUMLA ya watahiniwa 1,168,649 kutoka shule 20,019 Tanzania Bara wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) kesho na keshokutwa (Septemba 9 na 10, 2026), huku Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) likisisitiza uadilifu na ushirikiano wa jamii katika kuhakikisha mtihani huo unafanyika kwa amani na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 8, 2026, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Ally Mohamed, amesema kati ya watahiniwa hao, wavulana ni 531,467, sawa na asilimia 45.48, huku wasichana wakiwa 637,182, sawa na asilimia 54.52.
Amesema kati ya watahiniwa hao, 1,081,204, sawa na asilimia 92.52, watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, wakati 87,445, sawa na asilimia 7.48, watafanya kwa lugha ya Kiingereza.
Prof. Mohamed amesema watahiniwa 4,867 wenye mahitaji maalum nao wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo 82 wasioona, 1,551 wenye uoni hafifu, 999 wenye uziwi, 576 wenye ulemavu wa akili na 1,659 wenye ulemavu wa viungo.
“Katika mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, jumla ya masomo sita yatatahiniwa ambayo ni Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili.
“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huu yamekamilika…ikiwa ni pamoja na kusambaza karatasi za mitihani na nyaraka nyingine muhimu katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wasimamizi wa mitihani,” amesema.
Ameongeza kuwa, mazingira ya vituo vya mitihani yameandaliwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafanya mitihani katika hali ya usalama, utulivu na bila mianya ya udanganyifu.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kuwa usalama wa vituo vyote vya mitihani unaimarishwa na kwamba Vituo hivyo vinatumika kwa kuzingatia Sheria, Taratibu, Kanuni na Mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani Tanzania.
Vilevile, Prof. Mohamed amewataka watahiniwa kuepuka vitendo vya udanganyifu, akisisitiza kuwa NECTA haitasita kuchukua hatua dhidi ya atakayebainika kukiuka kanuni za mtihani.
“Baraza halitarajii kuona mtahiniwa yeyote akijihusisha na vitendo vya udanganyifu. Mtahiniwa atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani,” amesema.
Ameongeza kuwa jamii ina wajibu wa kushirikiana na Baraza katika kuhakikisha mtihani huo unafanyika kwa uadilifu, kwa kutoa taarifa za vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha uendeshaji wa mtihani.


