Na Atley Kuni, WAF – Morogoro
SERIKALI imezitaka mamlaka za miji, wataalamu, sekta binafsi na wananchi kuongeza juhudi katika usafi wa mazingira na udhibiti wa taka, baada ya kubainika kuwa Tanzania inazalisha jumla ya tani 689,144 za taka ngumu kila mwezi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Dkt. Samwel Nhiga, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa Mpango wa Haraka wa Usafi wa Mazingira na Mwongozo wa Kitaifa wa Usafi wa Mazingira na Uondoshaji wa Taka Ngumu nchini akirejea Kauli ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiwaapisha Viongozi wapya wa mikoa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, tani 339,095.2 sawa na asilimia 49.2 pekee ya taka zinazozalishwa kwa mwezi ndizo zinazokusanywa. Kati ya hizo, tani 325,087.6 sawa na asilimia 47.2 ndizo zinazofikishwa katika maeneo maalumu ya kutupa taka. Aidha, tani 350,048.8 sawa na asilimia 50.8 ya taka zote zinazozalishwa hazikusanywi, hali inayoonesha changamoto kubwa katika mifumo ya ukusanyaji, usafirishaji na utupaji wa taka.
Dkt. Nhiga alisema mrundikano wa taka usiodhibitiwa una athari kubwa kwa afya, mazingira na uchumi, kwa kuwa taka hutoa mazingira yanayofaa kwa mazalia ya nzi, mbu na panya wanaoweza kusababisha kuenea kwa magonjwa kama kipindupindu, malaria, homa ya matumbo (typhoid) na magonjwa ya kuhara. Pia, taka zinapotelekezwa katika maeneo yasiyo rasmi huathiri mandhari ya miji na kuchangia uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Tahadhari imechagizwa na na uwezekano wa mvua za El Nino, ambazo zinaweza kuongeza hatari ya mafuriko endapo taka, hususan plastiki, zitaendelea kutupwa ovyo na kuziba mitaro na mifereji ya maji. Mazingira machafu yanaweza pia kuongeza mazingira hatarishi kwa magonjwa kama kipindupindu, dengue, chikungunya, kuhara na homa ya matumbo, pamoja na kuongeza changamoto za malaria na minyoo.
“Serikali imeendelea kusisitiza utekelezaji wa mikakati ya kuboresha usafi wa mazingira, ikiwemo “Mita Tano Usafi Wangu, Usafi Wangu Mita Tano”, unaolenga kuhakikisha kaya, maeneo ya wazi, taasisi, miji, manispaa, majiji na wilaya vinakuwa safi” alisema, Dkt. Nhiga.
Dkt. Nhiga alisema hatua za haraka zinahitajika sasa ili kupunguza taka kwenye maeneo ya makazi na maeneo ya umma ili kuimarisha huduma za uzoaji wa taka na kuzuia uwepo wa madampo yasiyo rasmi.
Kwa upande mwingine, Dkt. Nhiga, aliwaasa viongozi na taasisi zinazohusika kusimamia ipasavyo huduma za usafi na mikataba ya watoa huduma za uzoaji taka kwani hatua hizo ni muhimu si kwa ajili ya afya pekee, bali pia katika kulinda taswira ya miji na nchi, hususan Tanzania inapojiandaa kwa AFCON 2027.









